Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WABUNGE 19 WALIOFUKUZWA CHADEMA WAFUNGUKA... HALIMA MDEE ASEMA KILICHOFANYIKA NI UHUNI MTUPU...MBOWE AJIBU UHUNI WAO


Baraza kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limetupilia mbali rufaa za waliokuwa wanachama wake 19 na kubariki maamuzi ya kuwafukuza uanachama yaliyofanywa na Kamati kuu ya chama hicho mwaka 2020.

Maamuzi hayo yamefikiwa usiku huu Mei 12,2022 kwenye kikao cha Baraza Kuu kilichoanza kufanyika Mei 11,2022 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.


Hata hivyo baada ya Baraza Kuu la CHADEMA kuunga mkono maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama hicho kuwavua uanachama wanachama wake 19, wanachama hao wakiongozwa na aliyewahi kuwa mbunge wa Kawe Halima Mdee wameonesha kupinga uamuzi huo.

Mdee ameelezea kutokubaliana na uamuzi wa Baraza Kuu la CHADEMA chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe wa kutupilia mbali rufaa zao za kupinga kufukuzwa uanachama na Kamati Kuu ya Chama hicho akisema kilichofanyika ni uhuni.

Mdee amesema hakukuwa na uhuru kwa wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho katika upigaji wa kura na hajaweka wazi kama kuna hatua nyingine watachukua baada ya maamuzi ya Baraza Kuu lakini amesisitiza kuwa hakukuwa na haki katika upigaji wa kura.

"Nakwepa kuzungumza maneno makali kwa sababu naheshimu viongozi wangu lakini sikujua CHADEMA umeanza kufanyika uhuni kwa kiwango hicho, Mimi ni CHADEMA naendelea kuwa CHADEMA lakini kilichofanyika pale ni uhuni wa kiwango cha hatari , nitaongea siku nyingine lakini kilichofanyika pale hata Mbowe anajua ni uhuni",amesema Mdee.


Mdee ambaye amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Kawe na wenzake 18 wamefukuzwa Chadema baada ya Baraza Kuu CHADEMA kubariki uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema kuwafukuza ndani ya chama kwa kukubali kwenda kuapishwa na kuwa wabunge kinyume cha matakwa ya chama hicho.


Katika mkutano wa Baraza kuu Idadi ya wajumbe walikuwa ni 423, Waliokubalina na maamuzi ya Kamati ya kuwafukuza Uanachama ni 413 sawa 97.6% na wasiokubaliana na uamuzi wa Kamati kuu ni 5 sawa na 1.2%, wasiofungamana na upande wowote ni 5 sawa na 1.2%

JE! NINI KINAFUATA BAADA YA KUVULIWA UANACHAMA?

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema amesema kwa sasa hakuna nafasi nyingine kwa waliokuwa makada 19 wa chama hicho ya kukata rufaa.


Amesema hatua inayofuata ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuandika barua ya kumtaarifu Spika wa Bunge kuhusu uamuzi uliofanywa na baraza kuu kwa hatua zaidi ikiwemo ya kutangazwa kuvuliwa ubunge.


Baada ya Mbunge Halima Mdee kwa niaba ya wenzake 18 kutokubalina na uamuzi wa Baraza Kuu la CHADEMA chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe wa kutupilia mbali rufaa zao za kupinga kufukuzwa uanachama na Kamati Kuu ya Chama hicho akisema kilichofanyika ni uhuni, Mbowe amemjibu na kuwaambia wao ndio waache uhuni.


“Nimesikitika hatujafurahia hali hiyo ila imebidi, maamuzi ya kuwafukuza yalifanyika tangu mwaka juzi kwenye kikao cha Kamati Kuu, kura zimepigwa mbele yao waache mambo ya kihuni”,amesema Mbowe.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com