DC NGUVILA: SIWEZI KUKUBALI HATA KIDOGO UVUVI HARAMU UENDELEE MULEBA...NITAPAMBANA NAO USIKU NA MCHANA


Mkuu wa Wilaya ya Muleba Toba Nguvila na Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi Magese Emmanuel Buleyi wakiteketeza nyavu haramu
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Toba Nguvila akizungumza
Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi Magese Emmanuel Buleyi akizungumza
Afisa mfawidhi wa Kituo cha ulinzi wa rasilimali za uvuvi Muleba Masanja Kadashi  akizungumza.

**


Na Mbuke Shilagi Kagera.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba Toba Nguvila amesema hawezi kukubali hata kidogo uvuvi haramu uendelee katika Wilaya yake ya Muleba na kwamba atapambana nao usiku na mchana kuhakikisha uvuvi haramu unaisha kabisa Wilayani humo.

Ameyasema hayo katika zoezi la uchomaji nyavu haramu katika mwalo wa Kimataifa Katembe Magarini Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera ambapo ilifanyika oparesheni tarehe 28 Aprili mpaka tarehe 3 Mei mwaka huu na kubaini zana haramu ambazo ni kokoro 81, Timba 663, Kamba za kuvutia kokoro Mita 10700 pamoja na nyavu zilizoboreshwa zinaitwa Kantwange zilikamatwa katika oparesheni hiyo.

Nguvila amesema kuwa zaidi ya wavuvi 52 wanao jihusisha na uvuvi haramu wamekamatwa na tayari wamefikishwa katika Vyombo vya Sheria na kwamba wale wanao kuwa wakihusika na uvuvi haramu ni wale wavuvi wadogo na wale wakubwa wamekuwa wakisubiri nje waletewe.

"Unapewa elfu mbili, tano au sita kuingia majini, alafu huyu anaye kupa nyavu haramu anaenda kunufaika huko, Kwanini usikatae uvuvi haramu, ukavua kwa nyavu halali ukapata samaki wa kiwango ambaye ukienda hata sokoni huwezi kuwa na wasiwasi", amesema Nguvila.

Amewataka wavuvi wote kukabidhisha zana haramu zote ziweze kuchomwa na kwamba wabaki na zana halali na kusema kuwa kwa wale wote watakao salimisha watasamehewa.

"Salimisheni makokoro yote ili ziwa lenu liwe salama" ,amesema Nguvila.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa uvuvi Wizara ya mifugo na uvuvi Magese Emmanuel Bulayi amesema kuwa kila mtu ana haki ya kulinda rasilimali ya Nchi yake na kwamba asilimia ya watu wamekuwa wakitegemea uvuvi.

"Kila mmoja akitengeneza wajibu yawezekana na inawezekana, na nikili tu hapa mbele yako Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya tukijipanga uvuvi haramu kukoma, tunaamua Leo na Wilaya ya Muleba iwe historia",amesema.

Kwa upande wake Jesca Edison ambaye ni mkazi wa Magarini ameishukuru Serikali kwa zoezi hilo na kwamba uvuvi haramu unapotokomezwa inasaidia wananchi kupata samaki zenye viwango bora vinavyotakiwa.

Naye Zephiline Mathias ambaye pia ni mvuvi amesema kuwa zoezi hili ni zuri na linasaidia kutunza mazalia ya samaki kwa miaka ijayo.

"Mimi Kama mvuvi nampongeza Mkuu wa Wilaya, kiongozi wetu kwa kulisisitiza hili, naamini kwamba watu waliobaki na nyavu haramu kama alivyosema Mkuu wa Wilaya kusalimisha, watasalimisha na kuendelea na uvuvi halali", amesema Zephiline.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post