Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WITO umetolewa kwa wabunifu mbalimbali mkoani kigoma kuongeza ujuzi kwa vitu wanavyobuni na kutengeneza ili viweze kuleta tija kwenye jamii na kurahisisha utendaji kazi.
Mwalim Joseph Joachim kutoka cha mafunzo na ufundi stadi (VETA) Kigoma alisema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya ubunifu ambayo kwa mkoa Kigoma ilitumika kutoa zawadi kwa mshindi wa shindano la ubunifu mkoa Kigoma.
Mwalim Joachim alisema kuwa wabunifu hao wanapaswa kuongeza ujuzi ili waweze kufika kwenye hatua nzuri zaidi ili kufanya kazi zao za ubunifu kuweza kutumika mbali zaidi ndani na nje ya nchi.
Katika hilo alisema kuwa ni muhimu kwa wabunifu hao kuwa na elimu ya ujasiriamali kwani ubunifu huenda sambamba na akili ya utafitaji maarifa zaidi ya kuongeza ubora wa kazi zao za ubunifu lakini kutafuta soko la nje la bidhaa zao za ubunifu.
Mchujo huo wa ubunifu ulioratibiwa na shirika la Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP ) pamoja na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yalikuwa na lengo la kutambua washindi na kutoa zawadi zitakazoendeleza ubunifu wao kwa kununua vifaa vya ufundi vyenye ubora zaidi.
Meneja wa SIDO mkoa Kigoma, Gervas Ntahamba alisema kuwa kupatikana kwa wabunifu wa shindano hilo na zawadi zinazotolewa zinalenga kutambua na kuendeleza vipaji vya wabunifu hao ili kupata mteja utakaowezesha kazi zao za ubunifu kuendelezwa kwa viwango vinavyokubalika ili ubunifu huo usilete madhara.
Ntahamba alisema kuwa wabunifu hao wanapaswa kwenda mbali zaidi katika kutengeneza bidhaa zao kwa wingi na kueleza changamoto zinazowakabili kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi katika suala la utaalam na fedha.
Mshindi wa shindano hilo, Stephano Bika kutoka halmashauri ya wilaya ya Kasulu ambaye ametengeneza pump ya maji yenye thamani ya shilingi 520,000 kwaajili ya usalama wa watoto na ulinzi wa mazingira alisema kuwa vifo vya watoto waliokuwa wakitumbukia visimani mara kwa mara ndiyo sababu iliyomfanya kubuni pumpu hiyo ya maji ili kuwaepusha watoto na hatari hiyo.
"Visima vingi vilikuwa wazi, maji yake ni machafu, wakati wa kuchota maji watoto hawana ulinzi kutoka kwa watu wazima, hii pump itawasaidia watoto kutumia wenyewe kuchota maji kwa usalama kwani ni nzuri, rahisi kutumia na haichafui mazingira" amesema Mshindi huyo wa ubunifu
Ameongeza kuwa alianza kutumia miti katika ubunifu wake lakini baada ya kupata ushindi wa pesa pamoja na mafunzo ya kuboresha ubunifu wake kutoka shirika la UNDP pamoja na SIDO aliiboresha pump hiyo ambayo mpaka sasa inatumia chuma.
Social Plugin