APOO CASTOR TINDWA AFUKUZWA KAZI YA UKURUGENZI WA HALMASHAURI



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Innocent Bashungwa amemsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara,  Apoo Castor Tindwa ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.

Waziri Bashungwa amechukua hatua hiyo leo Ijumaa Mei 06, 2022 wakati wa ziara yake mkoani humo na kutembelea Kituo cha Afya Genkuru na Hospitali ya Wilaya ya Nyamwaga kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kubaini ubadhirifu wa fedha takribani shilingi Milioni 704 za ujenzi wa miundombinu ya kituo cha Afya Genkuru na Bil. 1.4 za ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nyamwaga na Mkurugenzi huyo akiwa miongoni mwa watuhumiwa.


Bashungwa amesema haiwezekani Serikali ilete fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya ili kusogeza huduma bora karibu na wananchi halafu anatokea mtu anakwamisha jitihada za Serikali kwa maslahi binafsi, hii haivumiliki. Hata kama mtu amehama kituo alichofanya ubadhirifu tutamfuata huko huko aliko na atachukuliwa hatua.

Amewataka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuharakisha uchunguzi ili kubaini wote wanaohusika na ubadhirifu huo ili waweze kuchukuliwa hatua stahiki.

Aidha Waziri Bashungwa ameendelea kuwataka Wakurugenzi wa Halmashuri zote nchini kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo huku wakizingatia uadilifu na matumizi sahihi ya fedha za Serikali.

Mhe.Bashungwa yuko mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ambapo atatembelea Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Musoma Dc na Bunda Dc.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post