Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Mei 23,2022
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwanaume aliyejulikana kwa jina la Hamis Mayunga (27) mkazi wa Kijiji cha Dulisi wilayani Kishapu ameuawa kwa kupigwa risasi na anayedaiwa kuwa Mlinzi wa Kampuni ya Ulinzi ya Sam Security aitwaye Emmanuel Chacha katika eneo la Mgodi wa Almasi wa El – Hilal wilayani Kishapu.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumatatu Mei 23,2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando amesema tukio hilo limetokea Mei 20,2022 majira ya saa nne usiku katika eneo la mgodi wa El - Hilal.
“Hamis Mayunga (27) mkazi wa kijiji cha Dulisi wilayani Kishapu aliuawa kwa kupigwa risasi na Mlinzi wa Kampuni ya Ulinzi ya Sam Security yenye makao Makuu yake Mjini Shinyanga katika eneo la Mgodi wa El Hilal.
Huyu Hamisi Mayunga akiwa na wenzake wasiopungua 10 walikuwa wanavua samaki katika bwawa lililopo katika mgodi wa El – Hilal ndipo Mlinzi wa Kampuni ya Sam Security aitwaye Emmanuel Chacha akiwa na wenzake wanne waliondoka katika lindo lao walilopangiwa wakaenda katika bwawa hilo (ambalo siyo eneo lao la kazi, hawa hawafanyi doria) wakawazuia kuvua samaki , pakatokea kutoelewana ndipo akamfyatulia risasi kwa kututmia bunduki aina ya Shortgun ikampiga kwenye moyo upande wa kushoto na kusababisha kifo chake papo hapo”,ameeleza Kamanda Kyando.
“Mtuhumiwa wa mauaji Emmanuel Chacha alitoroka baada ya kutekeleza mauaji hayo na kutelekeza bunduki kwenye mlango wa mgodi. Tayari tunawashikilia walinzi wanne huku tukiendelea kumtafuta mtuhumiwa ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake”,ameongeza Kamanda Kyando.
“Natoa wito kwa walinzi wa makampuni binafsi ya ulinzi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kuacha kutumia nguvu kupita kiasi…Haiwezekani mtu anavua tu samaki, vipelege umpige risasi…Nimepanga kukutana na Makampuni binafsi ya ulinzi kwani hili sasa ni tukio la pili mwezi huu ambapo hata kule Mwakitolyo Mlinzi wa Kampuni ya Light Ndovu Security Abdul Chacha naye aliua mwananchi aliyekuwa anagombana na mke wake…Yaani mtu agombane tu na mkewe umpige risasi?”,amesema Kamanda Kyando.
Pia ametoa wito kwa wananchi wakiona eneo linalindwa wasiingie kwa nguvu.