Ofisa Mkuu Idara ya Fedha Benki ya Exim, Bw Shani Kinswaga (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu huduma mpya ya benki hiyo iitwayo ‘Exim Wajasiriamali Akaunti’ mahususi kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na wajasiriamali wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa huduma hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Wengine ni pamoja na Mkuu wa Bidhaa za Rejareja na Uhakika wa Mapato wa Benki ya Exim, Bi. Mtenya Cheya (Kushoto) na Meneja Msaidizi wa Bidhaa za Rejareja kutoka benki hiyo, Callist Butunga.
.........................................................
Benki ya Exim imezindua huduma maalum kwa ajili ya wafanya biashara wadogo wadogo na wajasiriamali ijulikanayo kwa jina la ‘Exim Wajasiriamali Akaunti’ ikilenga kusogeza karibu na kuhamasisha huduma za kibenki kwa makundi hayo muhimu.
Zaidi, hatua hiyo inatajwa kuwa inalenga kurahisisha uendeshwaji wa biashara miongoni mwa wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali wakiwemo mama ntilie, bodaboda, mafundi, wauza maduka na makundi mengine kwa kuwawezesha kuweka akiba kwa urahisi, kupokea malipo kwa njia za kidijitali sambamba na kuyaunganisha makundi hayo na fursa mbalimbali za kibiashara ikiwemo mikopo.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa bidhaa hiyo jijini Dar es Salaam hii leo, Ofisa Mkuu Idara ya Fedha Benki ya Exim, Bw Shani Kinswaga alisema pamoja na mambo mengine, huduma hiyo inaunga mkono wito wa serikali unaozihimiza taasisi za kifedha nchini kubuni huduma mbalimbali zinazolenga kuwasaidia wajasirimali na wafanyabiashara wadogo hususani vijana na wakina mama kujikwamua kiuchumi.
“Huduma hii mpya ni muitikio wa maoni ambayo tumekuwa tukiyapokea kutoka kwa wadau wetu mbalimbali wakiwemo wateja wetu. ‘Exim Wajasiriamali Akaunti’ ni huduma inayowapa urahisi wafanyabiashara wadogo iwapo hawajasajiliwa BRELA wakiwa na leseni ya biashara au TIN namba kufanya malipo mbali mbali ikiwemo njia ya mtandaoni, njia ya kadi, njia ya hundi na hata njia za kuhamisha pesa kutoka benki moja kwenda nyingine.’’ Alisema
Alisema huduma hiyo pia inakwenda sambamba na huduma ya Bima ya Maisha inayotolewa na benki hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Bidhaa za Rejareja na Uhakika wa Mapato wa Benki ya Exim, Bi. Mtenya Cheya alisema huduma hiyo ni maalum kwa ajili ya wateja wa sasa wa benki hiyo pamoja na wateja wapya.
“Pamoja na faida nyingine nyingi, bidhaa hii inalenga kuleta mabadiliko kwenye mtazamo wa ufanyaji wa biashara miongoni mwa wafanyabiashara wadogo na wajasirimali nchini. Lengo si tu kuyahamasisha makundi haya kufanya malipo kwa njia za kibenki bali pia huduma hii inawatengenezea taarifa nzuri ya kibenki inayoweza kuwapa nafasi ya kukopesheka kwani benki tayari inakuwa na taarifa ya mauzo yao na mahitaji yao tofauti tofauti ya kibiashara,’’ Alisema.
Akitaja baadhi ya faida zitokanazo na huduma hiyo Meneja Msaidizi wa Bidhaa za Rejareja kutoka benki hiyo, Callist Butunga alisema ni pamoja na urahisi wa kufanya malipo na viwango nafuu katika utoaji wa fedha kwa kutumia kadi sambamba na urahisi katika ufanyaji wa miamala kwa kutumia simu, mtandao au kupitia wakala.
“Pia huduma hii inawahakikishia wafanyabaishara wadogo kupata huduma zao kwa urahisi muda wowote, kufanya manunuzi mitandaoni na sehemu yoyote ya biashara. Akaunti hii inaweza kufunguliwa kwa shilingi ama dola, inaweza kufunguliwa kama akaunti ya pamoja na inamuwezesha mtumiaji kufanya malipo kwa kutumia hundi,’’.
“Hivyo basi tunawaamasisha wateja wetu wa sasa na wale wapya kufungua Exim Wajasiriamali Akaunti kwakuwa ina faida nyingi zaidi,’’ alisema.