MGODI WA BULYANHULU WAKABIDHI TREKTA WILAYANI NYANG’ HWALE KUFANIKISHA OPERESHENI YA USAFI WA MAZINGIRA


Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale ,Jamhuri David, (katikati waliokaa juu ya trekta mwenye miwani) akiwaongoza maofisa wa wilaya hiyo na Wananchi kupokea Trekta la kusomba taka lililotolewa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu.
**

Wananchi wakazi wa wilaya ya Nyang’hwale, ambao walikuwa hatarini kukumbwa na milipuko ya magonjwa kutokana na mlundikano wa takataka katika maeneo yao sasa wamepata ahueni kutokana na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, kukabidhi trekta ya kusomba taka kwa Halmashauri ya Wilaya hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 78 kupitia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (CSR).


Akiongea katika hafla ya kukabidhiwa trekta hiyo, Afisa Mazingira wa Wilaya ,Ezekiel Ntiryo, alisema “Tunaishukuru kampuni ya Barrick Bulyanhulu, kwa Msaada huu wa Trekta , tunaamini sasa hali ya usafi katika Wilaya yetu itaboreka kwa kiasi kikubwa,kwani matarajio yetu ni kuondoa taka mara mbili kwa wiki katika siku za Alhamisi na Jumatatu pia tunatarajia kuongeza huduma kwa maeneo ya miji inayokuwa kwa kasi kibiashara kama vile Bosolwa, Nyijundu, Bukwimba na Maeneo ya migodini.Kabla ya msaada huu wa Trekta hali ya Uzoaji wa Taka katika mitaa yetu ilikuwa chini ya asilimia 15% lakini baada ya msaada huu itafikia asilimia 65% iwapo tutaongeza juhudi.”

Mkuu wa Wilaya hiyo,Jamhuri David ,aliishukuru Barrick Bulyanhulu kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuleta maendeleo kwa Wananchi kupitia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (CSR), ambazo zimechangia kufanikisha miradi mingi ya maendeleo Wilayani humo na kufanya maisha ya wananchi kuwa bora.

“Leo tupo hapa kupokea Trekta ambalo limenunuliwa na kampuni ya Barrick Bulyanhulu, kwa gharama ya Shilingi Milioni 78, Trekta hili ni maalum kwa kazi ya kuzoa uchafu na kupeleka dampo, kwa kweli ni msaada mkubwa kwa wilaya yetu kwani kwa miaka mingi sana tumekuwa na changamoto juu ya uzoaji wa taka katika mitaa yetu ukichukulia kwamba mji wetu unakua kwa kasi na kupelekea uzalishaji wa taka kuongezeka kwa kiasi, ni matarajio yangu sasa mazingira ya Wilaya yetu yatakuwa safi, nichukue fursa hii kuwaomba wananchi kufanya usafi kila siku kwani tayari kwa sasa tunalo trekta ambalo litakuwa linasomba taka mara kwa mara”, alisema.

Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Idara ya Mahusiano kwa Jamii katika Mgodi wa Bulyanhulu, William Chungu, alitoa shukrani kwa viongozi wa Serikali na Wananchi kwa kuwa na uhusiano mzuri na Kampuni hiyo na kuongeza kuwa msaada wa Trekta lililokabidhiwa ni kwa ajili ya kusafisha mazingira. 

“Niwaombe ndugu zangu usafi ni jukumu letu sote,trekta hili tulitunze ili liweze kuboresha mazingira yetu ipasavyo ,milioni 78 ni pesa nyingi hivyo naamini tutakuwa tumefungua njia ya kuboresha mazingira ya usafi wilayani Nyang’hwale, haswa ikizingatia kampuni ya Barrick ni wadau wakubwa wa utunzaji wa mazingira”, alisisitiza Chungu.
Mwonekano wa Trekta mpya ya kusomba taka iliyotolewa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa Halmashauri ya Nyang'hwale kwa ajili ya kufanikisha zoezi la kusafisha Mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale ,Jamhuri David,(kulia) akishiriki zoezi la kuzoa taka baada ya kupokea trekta la kusomba taka lililotolewa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu.
Wafanyakazi wa Barrick wakifuatilia matukio katika hafla hiyo
Wananchi wakifuatilia matukio katika hafla hiyo
Wananchi wakifuatilia matukio katika hafla hiyo
Wafanyakazi wa Barrick wakifuatilia matukio katika hafla hiyo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post