Roboti akiwa kazini katika Hoteli ya Henn-Na
HEBU VUTA PICHA, unaenda hotelini na badala ya kupokewa na wahudumu, mapokezi unakutana na roboti lililotengenezwa kwa mfano wa mwanamke mrembo, linakukaribisha kwa maneno ya bashasha na kukuelekeza sehemu ya kusaini kwenye daftari, linakuelekeza namna ya kufanya malipo kisha linakupa funguo ya chumba.
Ni jambo lisilowezekana si ndiyo? Basi kwa taarifa yako, maendeleo ya sayansi ya teknolojia, yametufikisha hapa. Henn-na Hotel, imekuwa hoteli ya kwanza duniani kuhudumiwa na maroboti, ambapo huduma zote hotelini hapo, zimekuwa zikitolewa na maroboti ya aina mbalimbali.
Mapokezi kuna maroboti matatu, moja limetengenezwa kwa mfano wa binti mrembo wa Kijapan, na mengine yametengenezwa kwa mfano wa dragon. Sasa kinachofanyika ni kwamba, ukifika hotelini hapo, unapokelewa na roboti ambalo linazungumza kama binadamu, linakupa maelekezo yote muhimu na kuchukua hati yako ya kusafiria kwa wale wageni wanaotoka nje ya nchi, linaitoa copy na kukurudishia, kisha linakupa maelekezo kuhusu chumba utakachofikia.
Kama una mizigo, kuna roboti lingine ambalo kazi yake ni kubeba mizigo, unaelekezwa kwenye lifti na kwenda mpaka kwenye chumba chako. Ukifika unakuta tayari mizigo yako imewekwa mlangoni, unaiingiza ndani na kuendelea na ‘hamsini’ zako.
Pembeni ya kitanda pia kuna roboti lingine ambalo kazi yake ni kujibu maswali mbalimbali utakayokuwa unauliza. Litakuelekeza kuhusu nchi ya Japan, mahali kwenye vivutio vya utalii, ratiba za ndege na kadhalika. Ukitaka kuamka muda fulani, unalipa maelekezo na muda ukifika, linakuamsha kama ‘alarm’.
Roboti wakitekeleza majukumu yao kama wahudumu ndani ya Hoteli ya Henn-Na nchini Japan
Asubuhi kuna maroboti mengine yanayofanya kazi ya kupeleka vifungua kinywa kwa wageni, kila chumba. Unasikia mlango unagongwa na ukitoka, unakutana na roboti likiwa na sinia lenye kifungua kinywa.
Muda wa usafi ukifika, yanaingia maroboti mengine ambayo yatakusafishia chumba chako, yatabadilisha mashuka na kadhalika, yaani kwa kifupi ni kwamba shughuli zote zinafanywa na maroboti hotelini.
Hali hiyo imekuwa kivutio kikubwa kwa wageni kutoka maeneo mbalimbali duniani, kila mmoja akiwa na shauku ya kujionea.
Roboti akitoa huduma kwa mteja
Sasa kichekesho ni kwamba, hivi karibuni uongozi wa hoteli hiyo, uliamua kuyasimamisha kazi maroboti kadhaa, kutokana na uzembe kazini. Uzembe uliobainika ni pamoja na kutoa taarifa za uongo kwa wageni kuhusu vivutio mbalimbali vya utalii, kushindwa kutoa ratiba za ndege vizuri na kadhalika.
Watengenezaji wa maroboti hayo, wametakiwa kuyarekebisha kwanza kisha ndiyo yarudishwe kazini.
Ama kwa hakika, yajayo yanasisimua sana.
Social Plugin