Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia 14 kwa makosa ya kujihusisha na matukio mbalimbali katika jiji la Arusha, ikiwemo uporaji kwa kutumia pikipiki maarufu Tatu Mzuka.
Akitoa taarifa hiyo kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kamishina msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amesema Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha kuanzia Mei 19 2022 linaendelea na operesheni maalumu ya kupambana na wahalifu wanaotumia Pikipiki maarufu kwa jina la “TATU MZUKA” ambapo wamekuwa kero kwa wananchi katika mkoa huo kwa siku za hivi karibuni.
Amesema kuwa jumla ya watuhumiwa 14 walikamatwa katika operesheni hiyo kwa makosa ya kujihusisha na matukio mbalimbali katika jiji la Arusha, ikiwemo uporaji kwa kutumia pikipiki hizo maarufu tatu mzuka.
ACP Masejo amesema kuwa jumla ya pikipiki 12 zilikamatwa katika Operesheni hiyo huku mbili kati ya hizo zilikuwa hazina namba za usajili badala yake zilikuwa na plate namba iliyosomeka R.I.P SCOBER.
Amesema kuwa watuhumiwa hao wamehojiwa kwa kina na kukiri kufanya matukio ya uporaji na kwamba Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linaendelea na operesheni kali ya kuwatafuta watuhumiwa wengine waliotajwa.
Kamanda Masejo ametoa wito kwa wananchi hususani wazazi na walezi kuwapa malezi mema vijana wao ili kuepusha kutojiingiza katika uhalifu vile vile niwaombe wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu kwa Jeshi la Polisi.
Social Plugin