Muonekana wa madarasa mawili ambayo tayari yamekamilika
***
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema iwapo kuna mtu anadhani katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia kutakuwa na mlango wa kufanya ubadhirifu na kufuja fedha za umma, huyo atakuwa anajidanganya.
Shaka ameyasema hayo jana alipotembelea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kuhusu ujenzi wa miundombinu katika Shule ya Sekondari Ayalagaya Dareda wilayani Hanang mkoani Manyara.
“Nataka kuwaambia wanaodhani kuna mlango wa upigaji wa fedha za umma nataka kuwaambia kwamba hayo ni mawazo potofu na dhaifu mno, serikali ya Rais Samia iko makini na inafuatilia mienendo ya fedha hizo zinazotumika. Rais ameteua wasaidizi ambao moja ya jukumu lao la msingi ni kuhakikisha wanaishi na kufanyia kazi maono na dira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” amesema.
Amesema chini ya Rais Samia, fedha nyingi za miradi ya maendeleo imeshuka mpaka ngazi za chini na matunda ya fedha hizo yanaonekana, hivyo ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha fedha inayotolewa kwa ajili ya maendeleo inafanya kazi iliyokusudiwa kwa maslahi ya wananchi na kwamba haitarajiwi kuona zinatumika kinyume na mlango.
Amesisitiza Chama Cha Mapinduzi hakitasita kutoa ushauri kwa serikali kuchukua hatua dhidi ya yeyote ambaye atabainika kufuja fedha zinazotolewa na Rais Samia ambaye ana dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania katika kuwaletea maendeleo.
“Hapa Mkoa wa Manyara kuna miradi mingi imetekelezwa na taarifa zilizopo fedha zimetumika vizuri na hiki ndicho tunachotaka kusikia,” alisema.
Aawali akizungumza, Mkuu wa Wilaya Babati Lazaro Twange alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia madarakati, Halmashauri ya Wilaya ya Babati imepata manufaa mbalimbali ikiwemo kupatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.
“Hapa ndani ya mwaka huu wa fedha 2021/2022 tulipata fedha kwenye halmashauri hii moja ya wilaya ya babati ya kujenga madarasa jumla karibu 110, kuna madarasa 89 kwa ajili ya huu mpango wa maendeleo na mapambano dhidi ya uviko-19, lakini kuna madarasa 18 fedha kutoka serikali kuu, lakini kuna madarasa mengine zaidi ya 10 ambayo halmashauri wanayajenga kupitia mapato yao ya ndani.
“Kiufupi mwaka huu wa masomo 2022, mheshimiwa mlezi sisi tulilala usingizi tukisubiri kupanga wanafunzi waingie darasani,” amesema.
Moja ya bweni la Shule hiyo ya Sekondari ya Ayalagaya ambayo tayari limekamilika
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa Shaka Hamdu Shaka akifungua bomba la maji ndani ya moja ya chumba cha Maabara shule ya Sekondari ya Ayalagaya iliyopo mkoani Manyara jana Mei 15,2022.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa Shaka Hamdu Shaka akizungumza mbele wageni waalikwa na Wakiwemo Viongozi wa CCM alipkwenda kukugagua miundo mbinu ya shule ya Sekondari ya Ayalagaya iliyopo mkoani Manyara jana Mei 15,2022.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa Shaka Hamdu Shaka akifurahia jambo na Wanafunzi wa shule hiyo.
Social Plugin