Kauli hiyo ameitoa wakati alipomtembelea mtoto huyo katika wodi ya watoto Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja kutokana na kujeruhiwa na maji hayo.
Amesema ni jambo la msingi kwa jeshi hilo kushirikiana na Wizara yao kuona mtuhumiwa aliyefanya kitendo hicho cha unyama na cha udhalilishaji anakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Aidha amesema kumuunguza mtoto ambaye hana hatia haipaswi kuvumiliwa na kwamba inaonekana wazi aliyefanya tukio hilo hatoki maeneo ya mbali ya maeneo wanayoishi.
Amesema ikiwa jeshi hilo litatumia nguvu zao na utaalamu walionao hana shaka mtuhumiwa aliyetenda tukio hilo atakamatwa ili kuona haki ya mtoto huyo inapatikana .
“Naliomba jeshi lifanye kazi yake kwa nguvu zote naamini mnafanya kazi ila katika hili nawaombeni sana tuchukue hatua kuona mtuhumiwa anapatikana ili iwe mfano kwa wengine,” alisisitiza.
Waziri Riziki amesema binafsi yeye ni mzazi, analaani tukio hilo kwa nguvu zote na kuwaomba wanawake, walezi na wazazi kulaani vitendo vya aina hiyo ambavyo vina wadhalilisha watoto.
“Udhalilishaji sio kulawitiwa au kubakwa tu, kumhujumu mtoto wa jambo lolote lile nalo pia ni kumdhalilisha hasa ukizingatia maadili yetu ya kizanzibari hatuishi katika hatua kama hii,” amesisitiza Mhe, Riziki
Hata hivyo amewaomba madaktari kuendelea kumpa tiba mtoto huyo huku Wizara ikiendelea kushirikiana na familia na madaktari kuona kinachotakiwa katika usaidizi wanasaidia ili kuona mtoto huyo anarudi katika hali yake ya uzima na kuendelea na masomo yake.
Naye Muuguzi kutoka Wodi ya upasuaji na watoto walioungua, bi Rukia Seif Said amesema mtoto huyo wamempokea Mei 18 mwaka huu majira ya saa 7:00 za mchana akiwa na majeraha ya uso, mikono na katika bega.
Amesema hali ya mtoto huyo wakati anafikishwa hospitali hali yake ilikuwa sio nzuri na alipatiwa huduma ya kwanza na amekuwa akisafishwa vidonda vyake na hivi sasa anaendelea vizuri.
Kwa upande wake Mama Mzazi wa mtoto ambaye ameunguzwa maji ya moto naye hakutaka kutajwa jina lake amesema wakati mtoto wake akiwa amelala katika chumba chake usiku wa manane walisikia akipiga kelele na kusema maji ya moto na walipofika walimkuta ameshaungua katika sehemu ya uso na mkono.
Alisema wakati alipokwenda kugusa godoro alikuta maji ya moto ambayo yamepenya mpaka chini na walitoka kwenda kwa sheha kwa ajili ya kutoa taarifa.
Aidha alisema wakati tukio hilo linatokea hawakuweza kutoka kutokana na eneo wanalokaa hakuna hospitali na ilipofika asubuhi ndipo walipompeleka hospitali.
Social Plugin