Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SMZ KUHAKIKISHA WAFANYAKAZI WOTE WANAPATA STAHIKI ZAO KAZINI


Katibu Mkuu kutoka Afisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Khadija Khamis Rajab
Baadhi ya wasuluhishi wa migogoro wakiwa katika mafunzo
Juma Ali Makame msuluhishi migogoro
Mratibu Taifa wa sheria za kazi na viwango vya kazi kimataifa Maridadi Fanuel


Na Rahma Idrisa Haji - Zanzibar

Katibu Mkuu kutoka Afisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Khadija Khamis Rajab amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Itaendelea kushirikiana na Shirika la kazi duniani ILO kwa kuendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha Wafanyakazi na waajiri wote wanapata maslahi yao nchini.

Ameyasema hayo mara baada ya kufungua mafunzo ya siku 5 kwa wanasheria wa kitengo cha usuluhishi na uamuzi wa migogoro ya kazi Zanzibar, yaliyofanyika katika ukumbi wa Hotel ya Godern Tulip iliyopo uwanja wa ndege Wilaya ya Magharib B mkoa wa mjini Magharibi  nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Amefafanua kuwa katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza baina ya wafanyakazi na waajiri , pamoja na jamii kwa ujumla imefika wakati sasa kutoa mafunzo ambayo yatasaidia watoaji maamuzi ambao ni wanasheria kwa lengo la kutatua migogoro inayojitokeza katika sehemu za kazi kwa kutumia sheria na elimu walioipata .

"Tumefanya mafunzo haya kwa lengo la kutoa elimu kwa wasuluhishi na wamuzi wa migogoro ambapo kazi yao kubwa ni kusikiliza na kutatua migogoro mbali mbali inayojitokeza katika sekta za umma na serikali, binafsi , kwa sababu kadri siku zinavyokwenda maisha yanabadilika na maisha ya kufanya kazi yanabadilika katika sehemu ambayo migogoro inajitokeza katika kazi tofauti ,hivyo tumekuja na mbinu mpya ya kutatua migogoro ili waende na mabadiliko ya kidunia na nchi kiujumla",amesema.

Kwa Upande wake Mratibu Taifa wa sheria za kazi na viwango vya kazi kimataifa Maridadi Fanuel ameongeza kuwa lengo la kutoa Mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waamuzi kufanya maamuzi katika sehemu za kazi kupitia sheria za kazi za viwango vya kimataifa .

"Shirika la kazi Duniani ( ILO) limeandaa mafunzo haya kwa ajili ya waamuzi kutoka katika kitengo cha Usuluhisho na uamuzi kwa hapa Zanzibar nia hasa ya kufanya mafunzo kwa kushirikiana na Wizara ya kazi uchumi na uwekezaji ni kuwajengea uwezo waamuzi wa migogoro kuweza kutekeleza majukum yao kulingana na sheria .

"Sababu inapotokea mgogoro wa kazi sehemu yoyote kabla kuenda mahakama ya kazi ni lazima ianze katika kitengo cha usuluhisho na uamuzi ambacho kiko chini ya kamishna wa kazi kupitia Afisi ya Raisi kazi uchumi na uwekezaji hivyo ,Tumefanya mafunzo haya ili waweze kuelewa Utaratibu wa kesi zinapowafikia katika vitengo vyao vya kazi na kujua viwango vya kimataifa vinasemaje ili waweze kuamua kesi kulingana na utaratibu", amesema.

Juma Ali Makame ni msuluhishi wa migogoro ya kazi Zanzibar aliyepatiwa mafunzo hayo amesema kuwa mara baada ya mafunzo hayo ataweza kujua mbinu mpya ya kutatua migogoro .

Migogoro ya kazi Zanzibar ipo na inahitaji utatuzi wa mbinu na ujuzi mkubwa hivyo tunapopata mafunzo haya ya kutatua migogoro itasaidia kutatua kesi hizo",amesema .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com