MGEJA AFUNGUKA CHIMBUKO LA PANYA ROAD.... ASEMA NI "BOMU TULILOLIFUGA NA TUNAENDELEA KULIFUGA WIZARA TATU ZIKAE"


Khamis Mgeja

Mwenyekiti wa Tanzania Mzalendo Foundation Bwana Khamis Mgeja ameungana na Watanzania kupata mshtuko kwa kulaani kila kinachoendelea hivi sasa cha matukio ya kutisha nchini mpaka yanapelekea wananchi kuhatarisha maisha yao na kuporwa mali zao pia kujeruhiwa na kupewa ulemavu na kikundi cha uhalifu kinachoitwa PANYA ROAD.

Mgeja ameyasema hayo Mjini Kahama alipokuwa akiongea na waandishi wa habar ikuhusu matukio yanayojitokeza hivi sasa katika Jiji la Dar es salaam na baadhi ya maeneo mbalimbali nchini  kwa kundi lililoibuka la vijana wahalifu kwa jina maarufu PANYA ROAD  na sehemu nyingine hujulikana kama vibaka.


Mgeja amesema hali hii sio ya kupuuzia hata kidogo wala kukaa kimya wakati kikundi haramu cha vijana kinahatarisha maisha ya watu ikiwemo kujeruhi, lazima raia wema watoke na wasimame kutoa ushari ili Serikali  iyafanyie kazi mashauri hayo kwani hali hii ikiendelea Wananchi wataendelea kuwa na hofu kuhusu maisha yao na kuleta taharuki kwa hofu ya PANYA ROAD.


Mgeja amesema "Ni ukweli tuukubali au tusiukubali hali hii inavyojitokeza ni sawa na bomu tulilolifuga wenyewe na tunaendelea kulifuga, huenda huko mbele hali inaweza kuwa mbaya zaidi kuliko tunayoyaona hivi sasa, tutaona makubwa zaidi".


Hawa vijana haramu wanaojiita kwa jina haramu  maarufu  PANYA ROAD  ni zao au tunda la watoto wa Mitaani kwa jina maarufu huitwa machokora na wako pia vijana wachache wanaotoka katika familia".


Mgeja amesema hawa watoto wa mitaani (chokoraa) hivi sasa wamezagaa Mikoani kote nchini na hasa kwenye Miji, Halmashauri, Manispaa na majiji na wanazidi kuongezeka siku hadi siku liko wimbi kubwa sana endapo hakutakuwa na mkakati wowote au mpangilio mzuri na endelevu katika maeneo husika.


"Hawa watoto wa mitaani kutowaondoa au kutafuta njia yoyote ya kuwahifadhi tutakuwa tunaendelea kufuga bomu",amesema.


"Nawaomba Watanzania na viongozi kuanzia ngazi ya Mitaa, Kijiji, mpaka Taifa  tusingoje kila jambo Mhe. Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania mpaka aseme hata mambo ya PANYA ROAD (Chokoraa), naomba sana tumsaidie Mhe. Rais kwani sote tunajua ana majukumu mengi ya ujenzi wa Taifa iko haja kila mmoja wetu atimize wajibu wake na kujitathmini   ili  kulisaidia Taifa letu  na hasa hiki kizazi kinachorandaranda mtaani",amesema.


Mgeja ametoa masikitiko yake hivi sasa viongozi wengi wanasubiri mpaka matukio yatokee ndiyo wanajitokeza kuanza kusema sema akieleza kuwa huo ni udhaifu mkubwa sana kiuongozi.


"Kama hali hii ikiendelea na kujitokeza mara kwa mara naomba tusilaumiane wala kutafuta mchawi ila taasisi itaanza kunyosheana vidole na kupiga kelele kwa viongozi waliopewa dhamana ili wakubwa wao waliowakabidhi dhamana wasikie na kuona itakavyofaa dhidi ya viongozi hao.


"Hali hii ya ongezeko la watoto wa mitaani (chokoraa)  na hivi sasa tunda lake tunaliona linalo zaa PANYA ROAD tuliliona muda mrefu na kuwaeleza baadhi ya viongozi wenye dhamana na watendaji, tuliwapa ushauri jinsi ya kudhibiti hawa watoto lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa bali tulipuuzwa",amesema.


Mgeja ameeleza kuwa hawa watoto wa mitaani wengi wao hivi sasa wameanza kukua na wengine wamebarehe ni watu hatari sana kuwepo na jamii na kuwaacha wanazagaa mitaani.

 "Lazima tuelezane ukweli, nchi zingine huwavuna na kuwapeleka polini kujifunza mambo hatari sana ikiwemo uwasi, na ugaidi na wakitoka polini huwa  ni sawa na wanyama kwasababu hawana mjomba wala shangazi ndiyo haya yanayotokea nchi zingine za wenzetu tunaposikia kuna makundi ya waasi yako porini".


Mgeja ameishauri serikali kupitia ofisi ya Waziri mkuu mambo matano yafanyiwe kazi kama itampendeza Waziri Mkuu

1.  Halmashauri zitenge maeneo  ya vituo vya kuwafunza kazi, maadili, ikiwemo na ujuzi au wawaondoe mjini hawa vijana na kuwapeleka kwa wazazi wao kule waliko.

2.  Suala la ulinzi shirikishi

3.  Kuwepo mkakati wa viongozi wa Dini kuelimisha jamii jinsi ya kulea familia zao kimaadili hasa watoto.

4.  Halmashauri zote zitenge bajeti ya ulinzi na usalama kusaidiana na serikali kuu

5.  Kiwepo kikao cha pamoja cha Mawaziri Watatu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Tamisemi na Waziri wa Maendeleo ya jamii waweke mkakati wa pamoja wa kushughulikia kuzagaa kwa watoto mitaani kwani kila Wizara inaguswa kwa tatizo hilo.


Mgeja amesema anaimani na serikali hii ya awamu ya sita kuwa ni sikivu na kupitia kwa waziri mkuu matatizo haya yatashughulikiwa


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post