JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam limesema Diwani wa Kata ya Kawe, Mutta Rwakatare ambaye alikuwa hajulikani alipo tangu mwezi wa pili mwaka 2022 amefanikiwa kupatikana kwenye nyumba ya mwanamke.
Hayo yamejiri kufuatia hivi karibuni kujitokeza taarifa mbalimbali katika mitandao ya kijamii ikiwemo ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni kuwa, Diwani Mutta (43) mkazi wa Mikocheni Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuwa hajulikani alipo.
Akitoa taarifa leo kwa wanahabari jijini Dar es Salaam, Kamanda wa jeshi hilo Muliro Muliro amesema baada ya jeshi hilo kufanya ufuatiliaji wa taarifa hizo wamefanikiwa kumpata akiwa kwenye nyumba ya mwanamke aliyejulikana kwa jina la Ashura Ally Matitu (43) mkazi wa Tabata darajani.
Kamanda Muliro amesema, Ashura alidai kuwa Diwani huyo ni rafiki yake wa siku nyingi kwa zaidi ya miaka 10 na alifika nyumbani kwake Mei 19,2022 huku akiwa katika hali ya ulevi uliopindukia.
Amesema, kutokana na mazingira ya ulevi ambayo Diwani huyo amekutwa nayo na maombi yaliyotolewa na ndugu zake kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya matibabu, ndugu pia walitoa kumbukumbu za nyuma, mwenendo na tabia za diwani huyo.
Hata hivyo, Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi limemkabidhi diwani huyo kwa ndugu zake kwa matibabu na tiba zaidi za kisaikolojia.
Chanzo - Dira Makini
Social Plugin