Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADIWANI WATAKA WALIOKWAMISHA UJENZI WA MASOKO KIGOMA UJIJI KUADHIBIWA


Mkuu wa wilaya Kigoma Ester Mahawe akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani la manispaa ya Kigoma Ujiji kilichotoa azimio la kuendelea kwa ujenzi wa masoko ya Kigoma na Mwanga ambayo viongozi wachache wa masoko wanazuia ujenzi huo kwa maslahi yao. (Picha na Fadhili Abdallah )
Mkuu wa wilaya Kigoma Ester Mahawe akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani la manispaa ya Kigoma Ujiji kilichotoa azimio la kuendelea kwa ujenzi wa masoko ya Kigoma na Mwanga ambayo viongozi wachache wa masoko wanazuia ujenzi huo kwa maslahi yao.
Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Baraka Naibuha Lupoli (katikati) akizungumza kwenye kikao cha baraza la manispaa hiyo akitoa maazimio kuhusu Sakata la baadhi ya viongozi wa masoko kuzuia ujenzi wa masoko ya Kigoma na Mwanga mjini Kigoma.
Baadhi ya madiwani wa manispaa ya Kigoma Ujiji wakiwa katika kikao cha baraza hilo.
Baadhi ya madiwani wa manispaa ya Kigoma Ujiji wakiwa katika kikao cha baraza hilo.

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

BARAZA la madiwani katika halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji limeazimia kwa kauli moja kuendelea na mpango wa ujenzi kwa ajili ya maboresho makubwa ya masoko ya Kigoma na Mwanga yaliyopo manispaa ya Kigoma Ujiji huku wakitaka kuchukulia hatua kwa viongozi wa wafanyabiashara wanaokwamisha mpango huo.

Diwani wa kata ya Rusimbi,Bakari Songoro akiwasilisha ajenda maalum ya kujadili ujenzi wa masoko hayo kwenye baraza la madiwani la halmashauri ya manispaa ya Kigoma ujiji alisema kuwa ni jambo baya linalofanywa na viongozi hao wa masoko kuzuia mpango wa maendeleo wa ujenzi wa masoko hayo.

Songorio alisema kuwa kipindi cha nyuma mpango wa ujenzi ulikwama kwa sababu ya siasa kuwepo kwa idadi kubwa ya madiwani wa upinzani lakini leo baraza lina madiani 18 wa kata wa CCM na upinzani mmoja ikiwa na diwani mmoja wa kata yanakuja masuala ya kuzuia mipango ya maendeleo yanayosababishwa na viongozi ndani ya chama hicho.

Azimio hilo limetolewa kwenye kikao cha baraza la kawaida la madiwani kwenye halmashauri hiyo wakijadili ajenda maalum ya.

Mwenyekiti wa kamati ya mipango Miji ambaye ni Diwani wa kata ya Machinjioni manispaa ya Kigoma Ujiji,Himid Omari alisema kuwa ameshangazwa na kukwama kwa ujenzi wa masoko hayo licha ya taratibu zote za kisheria kufanyika ikiweo kuteua maeneo ya kuwahamishia wafanyabiashara hao kwa muda kupisha ujenzi, kukaa na wafanyabiashara kuzungumzia mpango huo na wafanyabiashara hao kukubali kuhama kupisha ujenzi.

Omari alisema kuwa baada ya kutaka kuanza utekelezaji wa mpango huo wameibuka watu wanaoitwa wafanyabiashara ambao wanazuia mpango huo ambapo uchunguzi wake umeonyesha kuwa baadhi ya viongozi wa masoko wanazuia mpango huo kwa maslahi yao binafsi.

Diwani wa kata ya Kasimbu, Fuad Seif aliwataja baadhi ya viongozi wa masoko ya Mwanga na soko la kigoma kuongoza mpango wa kuzuia ujenzi wa masoko hayo kutokana na kuwa na maslahi binafsi na kwamba mpango wa kuvunjwa na kujengwa upya kwa masoko hayo utaondoa maslahi yao na kushindwa kukusanya mapato hayo kama wanavyofanya sasa.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Rubuga,Omari Gindi (CHADEMA) amelaani vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wanaozuia mpango wa ujenzi wa masoko hayo kwa maslahi yao wakati mpango huo unalenga kuyafanya kuwa ya kisasa na kuongeza ukusanyaji wa mapato katika halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji.

Gindi alisema kuwa baadhi ya wananchi wa manispaa ya Kigoma Ujiji wamekuwa na tabia ya kuzuia miradi ikiwemo mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma ambao hadi sasa umekwama licha ya pesa kuwepo na kwamba jambo hilo lisijirudie kwenye ujenzi wa masoko hayo na kwamba Juni 30 ime mwisho na Julai Mosi masoko hayo yawe yamevunjwa.

Hamisi Bettese diwani wa kata ya Bangwe alisema kuwa wanaokwamisha mpango huo ni viongozi wa masoko ambao pia ni viongozi ndani ya CCM na kwamba jambo wanalofanya linakwamisha utekelezaji wa ilani na kutaka viongozi hao kuchukuliwa hatua ndani ya chama kwa vitendo wanavyofanya.

Viongozi hao wa masoko walitumiwa mwaliko wa kuhudhuria kikao hicho lakini hawakuhudhuria kikao hicho na diwani huyo alisema kuwa wiki iliyopita lilifanyika kongamano la nchi tano na wafanyabiashara waliohudhuria kongamano hilo wakataka kutembezwa kwenye masoko hayo lakini jinsi yalivyo sasa hakuna kiongozi ambaye aliambatana na wafanyabiashara hao kutembelea masoko hayo.

Naye Mkuu wa wilaya Kigoma, Esther Mahawe alisema kuwa anasikitishwa na mpango wa kukwamisha ujenzi huo wakati taratibu zote zimefanywa ikiwemo kukaa na wafanyabiashara hao na kuelekezana cha kufanya na hatua zote zimeridhiwa na pande zote.

Mwenyekiti wa CCM wilaya Kigoma Mjini, Yassin Mtalikwa alisema kuwa kama chama hawakubaliani na mpango wa kukwamisha ujenzi wa masoko hayo na watachukua hatua kupitia vikao vyao kwani huo ni kukwamisha utekelezaji wa ilani ya chama hicho.

Akihitimisha Mjadala huo Meya wa Manispaa ya Kigoma, Baraka Naibuha alisema kuwa wakati wa kongamano la wafanyabiashara alikuwa akikutana na Meya wa kalemie na Lubumbashi ambao walitaka kutembelea masoko hayo lakini kwa hali duni na miundo mbinu mibovu alikuwa akipiga chenga kuwapeleka kutembelea masoko hayo.

“Kwa kauli za madiwani ambao kwa kauli moja wameazimia mpango wa ujenzi uendelee tutaanza kuondoa vibanda na miundo mbinu inayomilikiwa na halmashauri kuanzia Ijumaa na ifikapo Julai Mosi tutaanza kuvunja vibanda vyote kutekeleza mpango wa ujenzi wa masoko hayo,”Alisema Meya wa Manispaa Kigoma Ujiji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com