SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson amepiga marufuku wabunge kufanya vituko kama kubinuka,kujiliza,kupiga magoti wakati wakichangia mijadala mbalimbali ndani ya Bunge.
Pia amepiga marufuku wabunge wa kike kuvaa nguo fupi zenye mpasuo, na wanaume ni mrufuku kuvaa nguo za kuwakawaka na zenye rangi kali bungeni.
Mheshimiwa Dkt.Tulia ametoa maelekezo hayo Mei 24, 2022 baada ya Mbunge wa Igalula, Venant Daud Protas kuomba mwongozo wa Spika akitaka kujua kama Bunge linaruhusu wabunge kuchangia mijadala kwa kufanya vituko ndani ya Bunge.
Mbunge Protas ameomba muongozo huo kufuatia Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Gregory Massay kupanda juu ya meza na kupiga sarakasi wakati akichangia mjadala ndani ya bunge Mei 23, 2022, tukio jingine limefanywa na Mbunge wa Viti Maalumu, Jacqueline Ngonyani Msongozi ambaye amepiga magoti wakati akiwasilisha hoja yake Mei 24, 2022 na Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Jerry Silaa kutokwa na machozi.
Awali Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay alipanda juu ya meza na kubinuka mtindo wa sarakasi bungeni jijini Dodoma ili kusisitiza kujengewa barabara ya lami maeneo ya Karatu, Mbulu, Hydom hadi Sibiti ambayo imekuwa kero ya muda mrefu kwa wananchi.
Mbunge huyo alisema ameisemea sana barabara hiyo, alilazimika kuruka sarakasi wakati akitoa maoni yake kwenye Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2022/2023.
“Mwaka jana wamesema kwenye bajeti wakasema watatangaza na nikataka kushika shilingi hapa sasa muda umepita mwaka mzima na hawatangazi hii barabara na kama wametangaza Wananchi wetu kule hawajui mwaka mzima umepita hilo tangazo linachukua muda gani na Wananchi wameniambia shilingi niichukue niende nayo Mbulu vijijini maana hakuna namna tena nikipiga sarakasi utanitoa nje na kama hunitoi nianze sasa hivi,”alisema Mbunge Massay.
Mbali na Flatei Massay, Mbunge wa Ukonga mkoani Dar es Salaam,Jerry Slaa naye ametokwa machozi bungeni akimlalamika Mkandarasi aliyepewa mradi wa mabasi ya mwendokasi huku kilomita 2.5 za mradi huo zikiwa chini ya kiwango huku pia Mkandarasi huyo akidaiwa kutolipa wafanyakazi na wazabuni jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Silaa alishikwa na uchungu huo na kumsababishia machozi wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi kwenye Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2022/2023.
“Mkandarasi huyu amepewa mradi wa mwendokasi kutoka Gongo la mboto mpaka Kariakoo haujakamilika Mkandarasi huyu ambaye kilomita 2.5 zimetinduka na zimeleta ufa kule Mbagala mkandarasi huyo asiyelipa wafanyakazi, wazabuni anaenda kuongezewa kazi nyingine na rais ameonya,”alidai Mheshimiwa Silaa.
Wakati huo huo,Mbunge wa Viti Maalum, Jackline Ngonyani Msongozi akiwa bungeni jijini Dodoma aliamua kupiga goti ili kushinikiza kujengwa kwa kivuko cha Mitomoni mkoani Ruvuma akidai vinatokea vifo vingi kutokana na kero hiyo.
Mheshimiwa Msongonzi amesema hayo wakati akichangia mjadala wa makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 ambapo amesema, watu wengi wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kuvuka katika mto huo kwa kutumia magome ya miti.
Amedai, hali hiyo inatokana na kukosekana kwa kivuko hicho kinachounganisha Wilaya ya Songea Vijijini na Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
CHANZO - DIRA MAKINI BLOG
Social Plugin