Msanii na mwanasiasa wa Upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, ameutaka uongozi wa CHADEMA kuwekeza nguvu katika kukuza vijana huku akisema anaamini vijana ndio wanaojua kupambana kudai haki zao.
Akihutubia katika kikao cha baraza kuu la CHADEMA, Mlimani City jijini Dar es salaam kiongozi huyo amesema ipo haja ya vyama vya siasa hususani vya upinzani kuwekeza kwa vijana na kuwafundisha siasa za mageuzi.
Aidha kiongozi huyo amewataka CHADEMA na wananchi wa Uganda kuungana katika kuendesha siasa za mabadiliko na mageuzi.
"Tunahitaji kuweka vichwa vyetu pamoja sisi Uganda na watu wa Chadema tupambane kuleta mageuzi katika nchi zetu hizi mbili, nipo hapa kuwaambia watu wa Uganda wanaelewa mnayopitia na nawaambia tupo pamoja katika kupambana", amesema kiongozi huyo
"Kwa kuwa tumezielewa changamoto zetu zinazotukabili na tumezikubali, tumeamua kujenga umoja na muunganiko wa kupambana kwa pamoja kama ambavyo imefanyika huko nyuma, tuchague kuwa kizazi kipya cha kupigania uhuru ndani ya nchi zetu" amesisitiza mwanasiasa huyo mpinzani mkuu wa Rais Museveni nchini Uganda.
Chanzo - EATV
Social Plugin