Wananchi wa kijiji cha Dulisi Kata ya Sekebugolo wakiaga Mwili wa Kijana Hamis Mayunga (19) ambaye alidaiwa kuuawa kwa kupigwa Risasi ndani ya Mgodi wa Almasi El-Hilali na Mlinzi wa Kampuni ya Sam Security Emmanuel Chacha.
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Kijana Hamisi Mayunga (19) mkazi wa kijiji cha Dulisi Kata ya Sekebugolo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, ambaye amedaiwa kuuawa na mlinzi wa kampuni ya Sam Security Emmanuel Chacha ndani ya mgodi wa madini ya Almasi El- Hilal, kwa kupigwa Risasi kifuani na kufariki dunia papo hapo hatimaye amezikwa leo nyumbani kwao, huku wadau wakiomba mauaji hayo yadhibitiwe.
Kijana Hamisi Mayunga aliuawa Mei 20 mwaka huu, wakati akiwa na wenzake wanne pamoja na kaka yake Robert Mayunga (21) wakiwa ndani ya Mgodi wa Almasi El-Hilali wakivua Samaki katika bwawa lililopo ndani ya mgodi huo, ndipo walipokamatwa na walinzi na kupigwa risasi.
Diwani wa Sekebugolo Frednand Mpogomi, akizungumza kwenye Mazishi hayo leo Mei 24, 2022, amesema kifo cha kijana huyo kimeumiza wananchi na kuviomba vyombo vya dola vitende haki juu ya kifo hicho.
“Tunalaani tukio la kifo cha kijana huyu na kimeumiza sana wananchi na hata wengine kuzirai na tumewakimbiza hospitali kupata matibabu na imani vyombo vya dola vitatenda haki juu ya kifo hiki, kijana alikuwa mdogo sana na tumepoteza nguvu ya Taifa,”anasema Mpongomi.
Naye Baba mzazi wa kijana huyo Mayunga Inegele, amesema mtoto wake hakustahili kifo hicho cha kikatili na kubainisha kuwa kama ni kosa kuingia ndani ya Mgodi huo wangewachukulia hatua kali za kisheria na siyo kumpiga Risasi huko ni kukiuka haki za binadamu.
Kaka wa Marehemu Robert Mayunga (21) ambaye walikuwa na mdogo wake ndani ya mgodi huo wa El-Hilal wakivua Samaki, anasimulia kuwa siku hiyo walikwenda kuvua Samaki majira saa moja jioni na walitega mitego yao kwenye bwawa hilo na ilipofika saa 4 wakaenda kuota moto kwenye kambi yao maeneo ya vichakani ndani ya mgodi huo na wakapitiwa na usingizi.
Amesema wakati wakiwa wamelala ilipofika majira ya Saa 6 usiku ndipo wakashtukia wamewekwa chini ya ulinzi, na walipoanza kukimbia ndipo ikafyatuliwa Risasi.
“Baada ya Risasi kufyatuliwa ilibidi nikimbilie ndani ya maji kwenye bwawa ambalo tunavua Samaki nikajificha humo, na walinzi walianza kunisaka kwa kumulika Tochi wakanikosa, na walipoondoka ndipo nikatoka na kukimbilia nyumbani, kumbe ile Risasi ilikuwa imempiga mdogo wangu,”amesema Mayunga.
“Kwenye mgodi huu siyo mara ya kwanza kuingia hua tunaingia mara kwa mara kuvua Samaki na walinzi wanatufahamu kabisa, lakini tuna shangaa siku hiyo sijui walipatwa na nini na kuamua kumuua mdogo wangu,”ameongeza.
Aidha, Mtetezi wa Haki za Binadamu John Myola kutoka Shirika la AGAPE ambaye ameshiriki mazishi ya kijana huyo, amelaani tukio hilo na kuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati juu ya matukio ya mauaji ambayo yanaendelea ndani ya mgodi huo wa El-Hilal juu ya walinzi ambao wanaulinda kwa kuendelea kukiuka haki za binadamu na kupoteza maisha ya vijana.
Amesema tukio hilo siyo la kwanza ambapo kuna vijana wengi wamepoteza maisha na wengine kupata ulemavu kwa kuendelea kupigwa na walinzi wa mgodi huo, ambapo Machi 10 mwaka huu kuna kijana mwingine mkazi wa kijiji cha Mwang’olo Cosmas Hamisi (25) naye aliuawa kwa kupigwa Risasi.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga ACP George Kyando, alikiri kutokea mauaji ya kijana huyo Hamis Mayunga kwa tuhuma za kupigwa Risasi na Mlinzi wa Kampuni ya Sam Security Emmanuel Chacha ambaye amekimbia mara baada ya kutokea mauaji hayo.
Amesema Jeshi hilo linamsaka mlinzi huyo, pamoja kushikilia wenzake wanne kwa ajili ya upelelezi zaidi, huku akionya walinzi wa makampuni binafsi wajiepushe na matumzi holela ya silaha na kusababisha mauaji.
Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE John Myola akiaga Mwili wa marehemu Hamis Mayunga, akiwa na wananchi wa kijiji cha Dulisi nyumbani kwao na kijana huyo kwa ajili ya mazishi.
Zoezi la kuaga mwili marehemu likiendelea.
Zoezi la kuaga mwili wa marehemu likiendelea.
Zoezi la kuaga mwili wa marehemu likiendelea.
Zoezi la kuaga mwili wa marehemu likiendelea.
Awali mwili wa marehemu ukiwasili tayari kwa mazishi.
Mwili wa marehemu Hamisi Mayunga ukipumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.
Mazishi yakiendelea.
Mazishi yakiendelea.
Mazishi yakiendelea.
Wananchi wakiwa msibani.
Wananchi wakiwa msibani.
Wananchi wakiwa msibani.
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Social Plugin