MAKATIBU UENEZI CCM WATAKIWA KUHAMASISHA WANANCHI KUSHIRIKI ZOEZI LA SENSA YA WATU NA MAKAZI


Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao
Mshauri wa Rais katika masuala ya siasa kwa upande wa Zanzibar Ali Haji Kirova

Na Rahma Idrisa Haji - Zanzibar
Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao amewaomba Makatibu Uenezi wa matawi ya CCM kuhakikisha wanawahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika tarehe 23 Mwezi Agosti mwaka huu.

Wito huo ameutoa leo wakati akizungumza na Uenezi kutoka ndani ya majimbo , matawi, wadi, mikoa pamoja na wilaya kichama katika mkutano mbele ya Waandishi wa habari katika ofisi kuu ya CCM Kisiwandui mkoa wa Mjini Magharibi.

Amewataka kuhakikisha kuwa wanawashajihisha wananchi na kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa sensa ndani ya jamii ili kila mwananchi kuweza kujua umuhimu wa sensa.

"Ni lazima muwashajihishe wananchi wote kujua umuhimu wa sensa kwani sensa inamanufaa makubwa ndani ya nchi yetu ikiwemo kuiwezesha serikali yetu kupanga mipango iliyokuwa bora na sahihi kwa watu wake",amesema.

Amesema kuwa kila baada ya miaka 10 serikali hufanya sensa lengo ni kuweka mipango yake sawa kupitia sekta za Kiuchumi, Kijamii, kielimu, Afya na Makazi hivyo kuna haja kubwa ya kila mwananchi kuweza kujua umuhimu wa sensa ili aweze kushiriki kwa kuhesabiwa.

" Ni lazima tuwafahamishe wananchi ndani ya majimbo yetu kuwa serikali itakapojua ina idadi ya watu wangapi kwa kila mkoa na wilaya hii itarahisisha zaidi kufanya mambo yake yote kwa mipango iliyomadhubuti kutokana na kuwa kila kitu hivi sasa kinaenda kidigitali", amesema.

Ameongezea kuwa sensa ni jambo la msingi kwa sababu huleta takwimu ambayo serikali hujua mahitaji ya wananchi waliomo ndani ya eneo husika lililohisabiwa kwa kufanya mambo mbali mbali kwa wananchi.

Katika hatua nyingine Nao amewaomba Makatibu Uenezi kumuunga mkono Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika jitihada zake mbali mbali anazozifanya ikiwemo kuwafahamisha wananchi juu ya miradi inayoendelea kujengwa katika mikoa na wilaya zao.

"Ni miaka miwili sasa tangu Dkt. Hussein Mwinyi aingie madarakani lakini maendeleo tumeanza kuyaona kupitia Ilani yake ya Chama Cha Mapinduzi ,miradi mingi imeanza kujengwa na mingine imekwisha kuzinduliwa Mjini na Vijijini ,hivi sasa tunaona Skuli zinajengwa , vituo vya afya vinajengwa pamoja na Miundombinu kuwekwa vizuri katika maeneo yetu ,hizi zote ni Jitihada za Serikali ya awamu ya nane katika kuhakikisha inawaletea maendeleo wananchi wake" ,amesema.

Kwa upande wake Mshauri wa Rais katika masuala ya siasa kwa upande wa Zanzibar Ali Haji Kirova amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kuongeza mishahara kwa watumishi ndani ya serikali kwa asilimia 16% hivyo amewataka wananchi kumuunga mkono katika kazi zake anazozifanya.

Nao baadhi ya Makatibu Uenezi wa matawi kutoka Chama Cha Mapinduzi walioshiriki mkutano huo walipata fursa ya kuielezea miradi mbalimbali iliyokwisha kamilika na inayoendelea kujengwa ndani ya majimbo yao huku wakimpongeza Rais wa Zanzibar kwa kujuhudi kubwa anazozifanya katika mikoa yote .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post