Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADIWANI BARIADI WALIA UHABA WA EFD MASHINE



Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.


MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu wamesikitishwa na uhaba wa mashine za kukusanyia mapato za kielektroniki (EFD-Machine) ambazo zimesababisha ukusanyaji wa mapato kuwa mdogo katika Halmashauri hiyo.


Aidha Madiwani hao wamemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo (Khalid Mbwana) kuchukua hatua kali kwa watendaji wa kata na vijiji ambao siyo waaminifu na wanakwamisha ukusanyaji wa mapato.


Hayo yamebainishwa kwenye baraza la Madiwani lililokutana kwa siku mbili kwa ajili ya kujadili taarifa za kata pamoja na maendeleo ya Halmashauri hiyo kwenye kikao cha robo ya tatu 2022 kilichofanyika makao makuu ya wilaya ya Bariadi-Dutwa.


Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mayala Lucas amesema mwezi May na June hali ya ukusanyaji wa mapato ni nzuri kwa sababu wamefikia asilimia 100 ya mapato ya ndani ambapo wamevuka lengo walilojiwekea.


‘’Mwezi May na June zaidi ya asilimi 100 tuliyojiwekea, tumezungumza na watendaji wanaokusanya mapato hali siyo nzuri wanaendelea lakini ukusanyaji siyo mzuri…tunahitaji kuwa na mashine za kielektroniki (POS) zaidi ya 50 lakini zilizpo ni 40, tumeweka utaratibu na mkurugenzi ili kupata zingine 10’’ amesema Mayala.


Diwani wa kata ya Mwadobana Duka Mapya Mashauri amesema Halmashauri ya wilaya ya Bariadi imezungukwa na halmashauri zingine na kwamba wamejiwekea mikakati ili kuhakikisha kila mwananchi anayekusanya mazao mchanganyiko anakatiwa ushuru kwa ajili ya maendeleo ya Halmashauri.


Amesema wananchi wanahitaji miundombinu ya barabara, madawa kwenye hospitali na kwamba bila ushuru halmashauri haiwezi kujiendesha wala kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo ina manufaa kwa wananchi.


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Juliana Mahongo amesema kuna udhaifu kidogo kwa wakusanya mapato ambao ni watendaji wa serikali ambapo Halmashauri inategemea mapato ya ndani ili iweze ujiendesha.


‘’Kwa uzembe huu kama utaendelea tutashuka kimapato, Mkurugenzi simamieni suala la ushuru, msionyeshe uzembe, kamati ya fedha kaeni muone namna ya kupata mashine za kukusanyia mapato ili tusiendelee kupoteza mapato’’ amesema Mwenyekiti huyo.


Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi Khalid Mbwana amesema halmashauri hiyo ilikuwa na mashine (POS) za kukusanyia mapato 53 kati yake 10 zimezuiliwa kutumika na Tamisemi na 2 ni mbovu.


‘’Kutokana na mwongozo, hatutakiwi kutengenezewa na mtu mwingine bali msambazaji na gharama za kutengeneza ni kubwa bora kununua zingine, hivyo tuna mashine 41 ambazo haziwezi kukidhi mahitaji kwenye kata 21’’ amesema na kuongeza.


‘’Tunaangalia maeneo muhimu, kama kuna kata haijapata mashine ya kukusanyia mapato tuwasiliane, tuna mkakati wa kununua mashine zingine 10, muhimu siyo kuwa na mashine bali tunaangalia ukusanyaji wa mapato ‘’ amesema.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Shigolile Chambitwe akiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani liliofanyika leo katika makao makuu ya wilaya hiyo Dutwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com