Basi lililopata ajali
Wananchi wakiwa katika eneo la ajali
Na Taikile Turo - Huheso Digital Blog
Watu wanne wamefariki dunia na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa katika ajali ya Basi la Abiria kampuni ya RUKSA CLASS baada ya kupinduka katika Kijiji cha Kayenze halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo wakati akizungumza na kipindi cha Morning Class (Darasa la asubuhi) cha Huheso Fm mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga amesema ajali hiyo imetokana na mwendokasi hali iliyompelekea dereva kushindwa kulimudu basi hilo kwenye kona.
Amesema waliofariki dunia ni wanaume watatu na mwanamke mmoja ambapo kati yao mmoja ni mwendesha baiskeli ambaye alikuwa pembezoni mwa barabara hivyo basi hilo lilimgonga na kupelekea kifo chake.
Kiswaga amesema ajali hiyo imetokea jana Mei 23, 2022 na waliojeruhiwa zaidi ya 30 wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa kuondoka lakini waliosalia ni wanne wanaoendelea na matibabu na miili ya marehemu ipo katika hospitali ya Wilaya ya Kahama.
Aidha, amewapongeza wananchi walijitokeza kwa ajili ya kushiriki uokoaji katika ajali hiyo sambamba na kuhakikisha ulinzi wa mali za abiria huku akiwataka kutoa taarifa za mwendokasi ili kuzuia uvunjifu wa sheria za barabarani.
Hata hivyo mkuu wa Wilaya Festo Kiswaga amewataka madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali huku akisema madereva wote watakaobainika kukiuka sheria watakamatwa na kunyang’anywa leseni zao kwa mjibu wa sheria.
Social Plugin