Waandamanaji wakiwa nje ya kasri la Sultan wa Sokoto, Muhammadu Sa’ad Abubakar
Serikali ya Jimbo la Sokoto nchini Nigeria, imetangaza marufuku ya kutotoka nje kwa muda wa saa 24 kuanzia leo, ili kukabiliana na maandamano na fujo za waandamanaji wanaotaka kuachiwa kwa wanafunzi wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kumuua mwanafunzi mwenzao, Deborah Samuel kwa madai ya kuikashifu dini yao.
Debora alipigwa na wanafunzi wenzake wa Chuo cha Shehu Shagari College of Education mpaka kuuawa kisha mwili wake kuchomwa moto kwa madai ya kuikashifu dini yao kwenye group la WhatsApp ambapo baada ya tukio hilo, polisi walianza kuwasaka waliohusika na mauaji hayo na kufanikiwa kuwakamata wanafunzi wawili huku wengine wakiendelea kusakwa.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi hawakuridhishwa na hatua hiyo ya polisi wakidai kuwa marehemu alistahili kuuawa, wakaanzisha maandamano ya kutaka wote waliokamatwa kuachiwa ara moja.
Katika taarifa iliyotolewa leo na Gavana wa Sokoto, Aminu Waziri Tambuwal, watu wote wanatakiwa kukaa majumbani mwao kwa saa 24 ili kupisha vyombo vya ulinzi na usalama kurejesha amani hususan katika Mji wa Sokoto na maeneo jirani.