Benki ya CRDB imeahidi uwezeshaji mkubwa kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara kati ya Tanzania na DRC kupitia bidhaa na huduma bunifu zinazotolewa na Benki hiyo. Ahadi hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB Congo, Jessica Nyachiro wakati wa Mkutano wa Uwekezaji na Biashara wa Tanganyika unaofanyika mkoa wa Kigoma.
Nyachiro alisema wafanyabiashara hao wakae mkao wa kula kwani Benki hiyo ipo katika hatua za mwisho za kufungua kampuni yake tanzu mjini Lubumbashi, Congo kabla ya mwisho wa mwaka huu huku akitanabaisha kuwa kuingia kwa Benki ya CRDB nchini Congo kutasaidia kurahisha biashara baina ya nchi hizi mbili.
"Ninawahakikishia wafanyabiashara wote katika Tanzania na Congo mwaka huu tutakuwa Lubumbashi," Nyachiro alisema kwa ujasiri huku akiongezea kuwa baada ya Lubumbashi benki hiyo itaenda Kinshasa kisha Uvira na Kalemi kwani mahitaji ya huduma katika sehemu hizo ni makubwa na vilevile ni maeneo ambayo kuna biashara kubwa na Tanzania.
Congo hadi sasa ina benki 16 zikiongozwa na Rawbank na kufuatiwa na Equity Bank, hivyo kuingia kwa Benki ya CRDB kutafanya idadi ya benki nchini humo kufikia 17. Nyachiro alisema kutokana na ushindani uliopo na mazingira ya biashara ya nchini Congo mkakati wa Benki ya CRDB ni kuwekeza zaidi katika mifumo ya kidijitali ya utoaji huduma ili kurahisha upatikanaji wa huduma kwa gharama nafuu na kuongeza ujumuishi wa kifedha.
Baadhi ya wafanyabiashara na wafanyabiashara wa Congo walisema wanaisubiri kwa hamu Benki ya CRDB nchini humo na wamekuwa wakitamani benki hiyo ipanue huduma zake nchini Congo muda mrefu. Meya wa Kalemi, Kakudji Kalama alisema wafanyabiashara wa pande zote mbili za Ziwa Tanganyika wanakabiliwa na changamoto nyingi za kibenki lakini ujio wa Benki ya CRDB nchini Congo utarahisisha shughuli za biashara.
"Ingawa benki itakuwa Lubumbashi, lakini ninaamini sheria na kanuni zetu zinaruhusu kupanua na kutoa huduma katika miji mikubwa. Mji wetu wa Tanganyika ndio lango la biashara nyingi za ziwa Tanganyika kutoka Tanzania...na tuna uhusiano mkubwa na Kigoma.," Bw Kalama alisema.
Baadhi ya wafanyabiashara walisema kukosekana kwa benki kama CRDB kunawawia vigumu kuhamisha fedha kutoka Tanzania kwenda DRC hivyo kukwamisha miamala ya kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.
Mfanyabiashara wa mafuta wa DRC, Bw Nondo Ibrahim, aliiomba benki hiyo kufikiria kuanza kubadilishana shilingi na faranga ili kuwaepusha na hasara na matatizo ya kubadilishana mizigo--kutoka faranga hadi dola na kisha hadi shilingi.
Kalama alisema kuwepo kwa Benki ya CRDB Congo pia kutawasaidia kutembea na fedha taslimu kwa ajili ya biashara jambo ambalo linahatarisha maisha yao na biashara kutokana na upotevu kwani kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakikumbana wanyang'anyi.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB Congo, Nyachiro alisema ubadilishaji wa shilingi na faranga unawezekana lakini unahitaji idhini ya Benki Kuu zote za nchi mbili. "Kwasasa tunapokea kwacha ya Zambia kwenye mpaka wa Tunduma. Hivyo tukishapata kibali inawezekana kwa faranga pia," alisema.
Benki ya CRDB imesema mkakati wake wa kufungua ukanda wa Ziwa Tanganyika umejikita katika kuweka mazingira wezeshi yabiashara na ujasiriamali, kusaidia ujenzi wa uchumi imara wa viwanda na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi.
Maeneo mengine ni Uwekezaji katika mifumo ya teknolojia itakayosaidia kuwezesha ukuaji wa biashara, kusaidia minyororo muhimu ya thamani ya kiuchumi na kukuza uwekezaji endelevu, pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Mbali na kukaribia kufungua kampuni tanzu nchini Congo, Nyachiro alisema Benki ya CRDB pia imeelekeza macho katika nchini za Zambia na Rwanda katika siku za usoni. Nyachiro alisema kampuni tanzu zitakazofunguliwa Lusaka na Kigali zinaendana na mpango mkakati wa benki hiyo wa kusaidia jitihada za serikali katika kukuza mahusiano ya biashara nan chi za jirani.
"Tunafanya kazi kwa karibu kwa ushirikiano na Benki Kuu za nchi hizi kuwezesha mipango yetu ya kuingia Zambia na Rwanda, alisema.
Social Plugin