Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WADAU WA MAENDELEO WAHAMASISHWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUWAWEZESHA WENYE ULEMAVU KUPATA ELIMU


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imewahamasisha wadau wa maendeleo waendeleo kuunga jitihada za kuhakikisha Watu wenye Ulemavu nchini wanapata haki ya elimu, kama ilivyo dhamira ya serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.


Tayari Ofisi hiyo tarehe 20 Mei, 2022, imefanikiwa kukarabati Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu cha Masiwani, jijini Tanga, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo; Nyota Foundation, Christian Blind Foundation (CBF), ASA Microfinane, Self-Microfinance, Desk and Chair Fundation, Reginald Mengi Foundation, Pangani Water Basin, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Halmashauri ya Jiji la Tanga.


Akiongea wakati wa Ufunguzi wa chuo hicho, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amewashukuru wadau hao kwa kuchangia ukarabati wa majengo na vifaa vya ufundi, pamoja na ununuzi wa vifaa vipya kwa ajili ya vijana wenye Ulemavu ambao watakuwa wakipata mafunzo ya ufundi stadi katika fani mbalimbali chuoni hapa.


Amefafanua kuwa Chuo hicho ambacho kilikuwa hakitoi mafunzo kwa Watu wenye Ulemavu kwa miaka 10, Mara baada ya kungiliwa kitakuwa na uwezo wa kupokea wanachuo 48 wa Bweni, wavulana na wasichana; na Wanachuo wa Wakutwa 55 jumla 103 wakiwemo pia wanafunzi wasio na Ulemavu ili kutekeleza azma ya kujenga jamii jumuishi.


Mhe. Katambi ameeleza kwa kufuatia uboreshaji wa miundombinu uliofanyika katika vyuo vingine vya Luanzari – Tabora, Yombo – Dar es Salaam, na Sabasaba – Singida idadi ya wanafunzi katika vyuo vya Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu umepanda kutoka Wanachuo 160 hadi 332 sawa na ongezeko la asilimia 107 katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2020/2021 na 2021/2022 hivyo kufanikisha kufikia lengo la kudahili wanachuo 400 kwa asilimia 83.


Aidha, Mhe. Katambi amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kutoa elimu bora na yenye usawa kwa wote bila malipo. Amekemea suala la kuwaficha Watoto wenye Ulemavu majumbani, kwakuwa Watoto hao wanakosa huduma na haki zao za msingi. Hivyo, ametoa rai kwa Watu wenye Ulemavu pamoja na wadau wanaojishughulisha na masuala ya elimu kuhakikisha Watoto wote wenye Ulemavu wanaandikishwa.


Amebainisha kuwa, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu kwa Watoto wenye Ulemavu kuanzia ngazi ya awali hadi Chuo Kikuu, ambapo kwa mwaka huu 2022 jumla ya Watoto wenye Ulemavu 2,883 wameandikishwa katika Elimu ya Awali wakiwemo Wavulana 1,470 na Wasichana 1,413, ngazi ya Msingi Wanafunzi 3,518 wakiwemo Wasichana 1862 na Wavulana 1,656 na Kidato cha Kwanza Wanafunzi 1,157 wakiwemo Wasichana 562 na Wavulana 595, ambapo kupitia mpango wa MEMKWA Wanafunzi wenye Ulemavu 122 wamesajiliwa ambapo Wasichana ni 67 na Wavulana 59.



Mhe. Katambi ameeleza kuwa Serikali imeelekeza Halmashauri zote nchini kutenga asilimia 2% ya mapato yake kwa ajili ya uwezeshwaji Watu wenye Ulemavu ambapo, katika mwaka wa fedha 2021/22 jumla ya shilingi bilioni 68.19 zimetengwa na Halmashauri zote nchini na kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1.94 zilitolewa kwa vikundi 382 vya Watu wenye Ulemavu.


Awali akiongea katika Ufunguzi huo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mjumbe wa Kamati hiyo, Zainabu Katimba, ameipongeza Ofisi hiyo kwa kutekeleza ushauri na maelekezo wanayoyatoa ikiwemo suala la kuboresha vyuo vya Watu Wenye Ulemavu nchini.


Katika Hatua nyingine, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bi. Pili Mnyema, amesema wataendelea kushirikiana na wadau hususani katika kutekeleza maombi ya chuo hicho ya kuhakikisha kuwa linapatikana eneo jingine la ujenzi wa chuo na eneo la chuo kilipo sasa linabaki kuwa Karakana.


Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Bi. Juyria Msuya ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa ukarabati wa Chuo hicho ambacho kinachukua wanafunzi wenye ulemavu na wasio na ulemavu kwa lengo la kutekeleza azma ya kujenga jamii jumuishi kama ilivyoelekezwa kwenye Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu pamoja na Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2013.


Wadau wa Maendeleo walioshiriki katika kuwezesha ukarabati wa chuo hicho, wakiongea kwa nyakati Tofauti akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, wameahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika masuala ya elimu, uwezeshwaji wa kiuchumi, afya, ajira, nyenzo za kujimudu pamoja na mafunzo ya ufundi stadi kwa Watu wenye Ulemavu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com