Mkurugenzi wa Makumbusho ya Azimio la Arusha Dkt Gwakisa Kamatula, akizungumza kwenye maandalizi ya mwisho ya Maadhimisho ya Makumbusho Duniani Jijini Arusha.
Maandalizi ya mwisho yakiendelea kuelekea Maadhimisho hayo Jijini Arusha
Mnara wa Mwenge moja ya kiashirio cha jiji la Arusha
............................
Na Sixmund Begashe
Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika Viwanja vya Makumbusho ya Azimio la Arusha, Jijini Arusha kusherekea siku ya Makumbusho Duniani ili kujipatia uelewa mpana wa mambo mbalimbali yanayohusu Urithi wa Utamaduni na Malikale uliohifadhiwa katika Makumbusho za Taifa.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Makumbusho ya Azimio la Arusha Dkt Gwakisa Kamatula, kwenye maandalizi ya mwisho ya Maadhimisho hayo Jijini Arusha na hasa wamejiandaa kikamilifu kupokea wageni wa ndani na nje ya Mkoa wa Arusha watakaoudhuria Maadhimisho hayo.
Dkt Kamatula amesema Kituo chake kimejiandaa vyema kuonesha nguvu ya Makumbusho kama Kaulimbiu ya Mwaka huu isemavyo katika kuhakikisha wanatoa huduma nzuri na bora kwa wageni wengi watakaokuja hasa wanaotokana na matokeo makubwa ya Filamu ya Royal Tour.
"Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kutuonesha njia kupitia Filamu ya Royal Tour, Makumbusho ya Azimio la Arusha tumejipanga kikamilifu kuhakikisha tunaitendea haki heshima hii aliyo tupatia Mhe Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan hasa katika utoaji wa huduma zetu nk". amesema Dkt Kamatula.
Dkt Kamatula ameongeza kuwa, Maadhimisho hayo yatapambwa na program za kielimu, Maonesho ya kudumu yaliyopo Makumbusho hiyo ya Azimio la Arusha na Maonesho ya Sanaa za Jukwaani kama Ngoma, Sarakasi, Muziki nk
Siku ya Makumbusho Duniani huadhimishwa Kila mwaka tarehe 18 Mei na Kaulimbiu ya Mwaka huu 2022 ni "Nguvu ya Makumbusho" hivyo Makumbusho ya Azimio la Arusha imeona iadhimishe tarehe 20 ndani ya wiki husika ili kutoa nafasi kwa watu wengi hasa wanafunzi na Wanavyuo kuudhuria.