***************
Na Alex Sonna-DODOMA
NAIBU Waziri wa Kilimo,Anthony Mavunde anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la pili la Tafiti za Ushirika linalotarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia Mei 11,2022 Jijini hapa.
Kongamano hilo litakuwa ni kwa ajili ya kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta ya ushirika kupitia tafiti zilizofanyika na uzoefu wa wadau mbalimbali.
Hayo yameelezwa leo Jijini hapa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) Dkt. Benson Ndiege wakati akitoa taarifa kuhusu kongamano hilo.
Dkt. Ndiege amesema kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) wamendaa Kongamano hilo ili kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta ya ushirika kupitia tafiti zilizofanyika na uzoefu wa wadau mbalimbali.
“Kongamano hili limeandaliwa kwa kushirikisha Wadau mbalimbali na linalenga kutoa fursa kwa watafiti pamoja na wadau wengine wa sekta ya ushirika kukutana na wanachama, viongozi na watendaji wa vyama vya Ushirika, ili kujadiliana matokeo ya utafiti na utatuzi wa changamoto zilizopo katika sekta hii.
“Kongamano la Pili la Tafiti za Ushirika litafanyika Jijini Dodoma kwa siku tatu kuanzia tarehe 11 – 13 Mei, 2022 kwenye ukumbi wa PSSSF.
“Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa kongamano hili atakuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde,”amesema Dkt. Ndiege
Dkt. Ndiege amesema tafiti mbalimbali zinazohusu sekta ya ushirika zimekuwa zikifanywa na wadau mbalimbali wakiwemo Vyuo vya Elimu ya Juu, Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali,Wadau wa Ushirika na wengine.
Amesema tafiti hizo zimekuwa zikitoa mapendekezo ya utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazokabili maendeleo ya Ushirika nchini.
Hata hivyo,walengwa wakubwa ambao ni wanachama, viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika wamekuwa hawapati fursa ya kupata matokeo ya tafiti hizo na mapendekezo yake.
Aidha,amesema tafiti nyingi zimekuwa zikichapishwa kwenye majarida ya Kitaaluma, Mitandao na mara nyingi kuandikwa kwa lugha ya kiingereza; lugha ambayo siyo rafiki kwa wanaushirika wengi; hivyo mapendekezo mengi yamekuwa hayafanyiwi kazi.
“Hivyo, tunawakaribisha washiriki wote katika Kongamano hili muhimu kwa Maendeleo ya Sekta ya Ushirika nchini,”amesema.
Social Plugin