NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeibuka mshindi wa jumla katika maonesho ya afya na usalama mahala pa kazi jijini Dodoma.
Maonesho hayo ya afya na usalama mahala pa kazi yameratibiwa na Wakala wa Afya na Usalama Mahala pa Kazi nchini (OSHA) jijini Dodoma katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Afya na Usalama Mahala pa Kazi ambayo huadhimishwa duniani Aprili 28 kila mwaka.
Pia OSHA wameipatia pia GGML tuzo ya kampuni bora inayoifikia zaidi jamii katika
uelimishaji wa masuala ya afya na usalama
kwenye maeneo yao.
Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Afya na Usalama Mahala pa Kazi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako ameipongeza kampuni ya GGML kwa kutoa kipaumbele kwenye afya na usalama wa wafanyakazi na kutoa wito kwa kampuni nyingine nchini kuwekeza katika kuboresha mazingira ya afya na usalama wa wafanyakazi wao.
“Waajiri wengi nchini hawatoi msisitizo kwenye masuala ya afya na usalama kwa sababu ya kuogopa gharama. Lakini linapokuja suala la ajali na vifo, gharama huwa ni kubwa zaidi na kuwaathiri waajiri wenyewe, kampuni, wafanyakazi, jamii, taifa na uchumi kwa ujumla.
“Tuendelee kushirikiana kujenga utamaduni bora wa afya na usalama mahala pa kazi kama kauli mbiu ya siku ya afya na usalama mahala pa kazi mwaka huu inavyosema,” aliongeza Profesa Ndalichako.
Aidha, Meneja Mwandamizi wa GGML anayeshughulikia masuala ya afya, usalama, mazingira na mafunzo Dk. Kiva Mvungi alisema siri ya kampuni ya GGML kuibuka kidedea katika masuala ya afya na usalama kwa muda mrefu ni kuwa na utamaduni bora wa kushirikisha wafanyakazi na wakandarasi katika kuenzi tunu ya afya na usalama mahala pa kazi.
“Changamoto ya ajali na vifo mahala pa kazi ni suala linaloathiri wafanyakazi wengi duniani pamoja na familia zao. Tumejitahidi kuzuia vifo na ajali katika mgodi wetu ndiyo sababu hatujapata ajali ya kuondoa maisha ya mfanyakazi ndani ya mgodi kwa zaidi ya miaka 10 hivi sasa.
“Mara ya mwisho mtu kupata majeraha yaliyomzuia kuendelea na kazi ilikuwa mwaka 2018 wakati mwaka 2017 tulipata tukio moja la mtu kupata jeraha dogo lilomzuia kuendelea na kazi.
“Hii kwetu ni rekodi nzuri ukilinganisha na migodi mingine na tunaendelea kuwaelimisha wafanyakazi wetu kuendelea kuwa makini na kufuata taratibu zote za usalama wanapokuwa kazini ili tuhakikishe tunaendelea na rekodi yetu ya kuwa mgodi kinara katika kuzingatia usalama kuliko migodi yote duniani,”alisema Dk. Kiva Mvungi.
Alisema miongoni mwa kampuni zote za AngloGold Ashanti ambayo ni kampuni mama ya GGML imeendelea kuwa kampuni bora ya kwanza inayozingatia usalama kwa kiwango kikubwa.
Ameongeza kuwa kampuni ya GGML inathamini maisha ya wafanyakazi na wakandarasi wake na ndiyo maana imeweka suala la usalama kuwa kipaumbele chake cha kwanza katika shughuli zake.
“Tumekuwa tukishirikiana na OSHA kila mwaka kuielimisha jamii na taasisi zinazoshiriki katika maonesho haya mifumo na teknolojia za kuboresha afya na usalama sehemu zetu za kazi.
“Lengo ni kuikumbusha jamii kuwa maisha na uhai ni jambo la msingi kuliko hata uchumi au faida ambayo inaweza kuzalishwa na kampuni,” alisema Dk Kiva Mvungi.
Katika maonesho ya afya na usalama mahala pa kazi mwaka jana, GGML iliibuka mshindi wa pili.
Mapema mwaka huu, GGML iliibuka mshindi wa jumla katika kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini Tanzania kwa mwaka wa fedha 2020/2021 baada ya kunyakua tuzo katika vipengele vya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, mazingira, usalama, mlipaji bora wa mapato (kodi) na uendelezaji wazawa, ikiwa ni mara ya pili mfululizo.
Xxxxxx
CAPTION
4.
Social Plugin