Msajili Msaidizi wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Christine Metimura akila kiapo cha nafasi ya Naibu Msajili katika mahakama hiyo mbele ya majaji wa mahakama ya rufaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Na Agness Nyamaru,Arusha.
Jaji mstaafu wa mahakama ya rufaa ya Tanzania , Edward Rutakangwa amewataka wasajili wote nchini kuwa wakweli kwa majaji wao ili haki iweze kutendeka ipasavyo.
Ameyasema hayo leo Mei 6,2022 katika hafla ya uapisho wa Naibu Msajili kwenye mahakama ya haki ya jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ) na kusisitiza kuwa ni vyema wasaidizi wakawa wa kweli huku wakijitahidi kusoma sheria za mahakama kwani bila kujua sheria hizo hawawezi kufanya shughuli za usajili mahakamani.
"Muda wote wanatakiwa kusoma sheria za mahakama kwani katika mahakama zote sheria na kanuni za mahakama ndio bibilia zetu na misaafu yetu bila kijua sheria hizo huwezi kufanya kazi za usajili sawasawa,"alisema Jaji huyo mstaafu.
"Mahakama ni chombo muhimu katika kukuza mahusiano ya kisasa,uchumi na tamaduni katika Afrika Mashariki ikiwa ni sambamba na kuwepo na wafanyakazi ili kufanya kazi kwa weledi.
"Kama mahakama haina wafanyakazi,vitendea kazi hutuwezi kutegemea tupate haki ya haraka kama vision yetu inavyojieleza hivyo kupitia msajili huyu mpya tunaimani baadhi ya changamoto zinaweza kuondoka na bila kuwa na msajili kazi za mahakama zitasimama," alisema Rutakangwa.
Jaji Rais wa mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Nestor Kayobera alisema kwa takribani miaka sita walikuwa hawana msajili katika mahakama hiyo ya rufani kutokana na msajili wa awali kustaafu hivyo kuchaguliwa kwa Naibu msajili huyo kutaleta afueni katika utendaji wa kazi zao.
Alisema bila kuwa na msajili wa mahakama wala naibu wake changamoto nyingi hutokea hivyo wameliomba baraza la mawaziri la jumuiya ya Afrika mashariki kufanya mchakato wa leta msajili kamili ili kufanya kazi kwa weledi unaotakiwa.
Aidha Christine Metimura ni mteuliwa katika nafasi hiyo na naibu msajili katika mahakama hiyo alisema anatarajia kufanya kazi zake kwa bidii na kufikia malengo ya jumuiya kwa kusaidia wanachama wa jumuiya hiyo kupata haki zao kwa wakati.
Social Plugin