RAIS SAMIA ATOA MILIONI 10 KWA KILA MKOA KUSAIDIA MACHINGA

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo amezungumza na viongozi wa shirikisho la umoja wa Machinga na kuwaeleza kuwa Serikali yake itaendeleza ushirikiano kwako na kuahidi kuwapatia Shilingi milioni 10 kila mkoa .

Na Dotto Kwilasa, DODOMA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahakikishia  Wamachinga nchini kuwa katika mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai Ofisi yake kupitia Tawala za mikoa na Serikali za mitaa itatoa Sh. Milioni 10 kwa kila mkoa  kuwezesha shughuli za machinga nchini.


Rais Samia amezungumza hayo leo kwa njia ya simu wakati mkutano wa mafunzo ya Viongozi wa Machinga Tanzania (SHIUMA) yakiendelea Jijini hapa na amewahakikishia kuwapa ushirikiano Wamachinga nchini kwa kufanya kazi zao bila bugudha kwenye  mazingira mazuri.


"Nakushukuru Waziri kwa kuwapa  Wamachinga Ofisi ambayo ni jengo la Serikali,nimesikiliza hotuba yao na nimefurahishwa,nawahakikishia ushirikiano na mazingira mazuri na ifikapo mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai nitatoa milioni kumi kwa Kila mkoa kuwezesha shughuli zao,"amesema.

Awali katika mkutano huo ,Naibu Katibu Mkuu (SHIUMA) Joseph Mwanakijiji amebainisha kuwa kwa sasa wana mahusiano mazuri na serikali jambo linalosaidia Machinga anakuwa na mazingira mazuri na kuhakikisha anapangwa vizuri na kufanya biashara kwa uhuru.

"Tuna changamoto nyingi lakini kero ya miundombinu kwa baadhi ya masoko haiko sawa na kusababisha kiuchumi hatufikii malengo,baadhi ya miundombinu haiko sawa na kuhatarisha afya,ukosefu pia wa ofisi za Machinga na changamoto za kibajeti,"ameeleza.


Amezitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na stadi za biashara ,makazo bora,umilikishwaji wa maeneo ya machinga na kuomba kupewa barua ya idhini kuepuka kuondokewa mara kwa mara pindi halmashauri zinapo badili matumizi ya maeneo.


Mafunzo hayo ya Viongozi wa shirikisho la umoja wa Machinga Tanzania yameandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya jamii,Jinsia,wanawake na makundi maalumu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo huku kaulimbiu yake ikiwa "Machinga ni fursa sahihi ya kukuza uchumi wa nchi yetu".

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post