Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila
NA GODFREY NNKO
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa David Kafulila amechukua uamuzi mgumu wa kuwatimua kazi maofisa ushirika wa halmashauri sita.
Halmashauri hizo ni Bariadi Mjini, Bariadi Vijijini, Maswa, Busega,Itilima,Meatu zote za Mkoa wa Simiyu.
Sambamba na kuvunja uongozi wa AMCOS 335 huku akisisitiza kuwa,bei ya pamba mkoani Simiyu inakwenda kuvunja rekodi ya miaka 30.
Mheshimiwa Kafulila ameyasema hayo leo Mei 5, 2022 huku akieleza kuwa, zao la pamba Mkoa wa Simiyu linapaswa kuheshimiwa na watu wote.
"Kwanza inafahamika Simiyu ndio Simba wa Pamba Tanzania ikizalisha wastani wa asilimia 40 hadi 60. Pamoja na bei nzuri msimu uliopita kufikia shilingi 1800, bado kuna malalamiko mengi yaliyothibitika mchezo mchafu kati ya AMCOS na Maofisa Ushirika uliosababisha mkulima kutopata bei halisi iliyolipwa na mnunuzi.
"Aidha uchunguzi wa PCCB (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kuhakiki kila AMCOS kuona vielelezo kuthibitisha malipo aliyolipwa mkulima na kiasi ambacho AMCOS iliuza pamba kwa niaba ya mkulima.
"Mpaka sasa zimechunguzwa AMCOS 189 na zote hakuna vielelezo kuthibitisha malipo sahihi kwa mkulima,"ameeleza Mheshimiwa Kafulila.
Kwa kuzingatia changamoto hizo na zaidi maelekezo ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kutaka kusafisha mfumo mzima wa usimamizi zao la pamba hasa katika msimu huu ambao makadirio ya Bodi ya Pamba yanaonesha Simiyu itavuna zaidi ya mara tatu ya msimu uliokwisha kwa kupata kati ya tani 250,000 mpaka 300,000, kiasi ambacho hakijawahi kupatikana hata ukiunganisha na Shinyanga,RC Kafulila alieleza yafuatayo kama mwelekeo mpya wa usimamizi wa manunuzi ya pamba msimu huu unaonza Mei 20.
" Kwanza, ili kuimarisha uwajibikaji wa AMCOS,Tumekubaliana na Mhe. Waziri kuwa uongozi wote wa AMCOS zote unafutwa na hivyo uchaguzi utarudiwa ndani ya wiki moja.
"Pili, ili kuhakikisha uchaguzi huo unaleta viongozi thabiti, wakulima wote wa pamba kwenye kijiji husika watakuwa na haki ya kushiriki uchaguzi. Hii inatokana na ukweli kuwa wanachama wa AMCOS hawazidi asilimia 30% ya wakulima wote. Hivyo asilimia 70% ya wakulima ambao sio wanachama wa AMCOS washiriki uchaguzi huo. Haki hii pia inachangiwa na ukweli pia kwamba AMCOS zinalipwa shilingi kwa kila kilo ya pamba bila kujali ni pamba ya mwanachama au asiye mwanachama wa ushirika( AMCOS).
"Tatu, ili kuongeza uwazi, wakati wa manunuzi msimu huu unaoanza Mei20, 2022, kila AMCOS itapaswa kuweka wazi kwenye kituo cha manunuzi bei ya kila mnunuzi aliyewapa pesa wamnunulie pamba ili wanunuzi watakaonunua pamba kupitia AMCOS wajue kwanini wanapata au wanakosa kulingana na bei zao wanazotaka AMCOS iwanunulie pamba.
"Nne, ili kuhakikisha usimamizi thabiti, amelekeza wakurugenzi Halmashauri kuwaondoa maofisa ushirika wote ngazi ya wilaya na kupangiwa kazi zingine na taratibu za kuweka maofisa wengine zifanyike ndani ya wiki moja.
"Tano, ili kuongeza uwazi na ushindani wanunuzi binafsi wataruhusiwa kuweka mawakala wao kwenye soko la pamba na kushindana na AMCOS katika masoko hayo vijijini na wote AMCOS na mawakala wanunuzi watasimamiwa na Serikali ya kijiji chini ya mtendaji wa kijiji. Hivyo Mtendaji wa Kijiji ndio Msimamizi Mkuu wa uuzaji wa pamba akishirikiana na AMCOS.
"Sita, ili kuhakikisha usimamizi thabiti, pamba yoyote halali itapaswa kuwa na iliyouzwa kwa bei sawa au zaidi ya bei elekezi na iwe na kibali kilichothibitishwa na mtendaji wa kijiji na AMCOS pamba iliponunuliwa. Saba, Makatibu wote wa AMCOS watapaswa kutoka ndani ya kata husika.
"Nane, mkulima atakuwa na uhuru wa kuuza Pamba kwa AMCOS au Wakala wa Mnunuzi binafsi ambao wote watakuwa kwenye soko la pamba chini ya Mtendaji wa Kijiji.
"Tisa, wanunuzi wa pamba takuwa na uhuru wa kununua pamba kupitia AMCOS au Wakala wake lakn manunuzi yote yatasimamiwa na serikali ya kijiji. Wote, AMCOS na Wakala wa Mnunuzi watanunua pamba kwenye soko ndani ya Kjiji na VEO atakuwa na Msimamizi Mkuu,"amefafanua Mheshimiwa Kafulila.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Kafulila amewataka wakulima na wananchi wote kutoa ushirikiano hasa ikizingatiwa kuwa usimamizi thabiti wa Serikali utaendelea kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri.
"Nimeshiriki kikao cha wataalamu wa Bodi ya pamba, Ushirika na Wanunuzi wa pamba msimu huu kwa lengo la kuhakikisha mkulima anapata bei inayofanana na jasho lake. Najua Waziri atatangaza bei elekezi Mei 20, lakini ninachoweza kuwahikishia wakulima ni kwamba bei itakuwa nzuri kuliko miaka yote katika kumbukumbu za pamba tangu mwaka 1990,"amesema Mheshimiwa Kafulila.