Meneja wa Ewura Kanda ya Kaskazini Mhandisi Lorivii Long'idu akitoa elimu ya gesi za majumbani kwa Wakala na Wasambazaji wa Gesi za Kampuni ya Taifa.
Na Rose Jackson,Arusha
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kaskazini imewataka wauzaji wa gesi za kupikia kuhakikisha wanakuwa na mizani za kupima gesi kwani kutokuwa na mizani ni kosa la kisheria.
Hayo yamesemwa na Meneja wa EWURA Kanda ya Kaskazini Mhandisi Lorivii Long'idu wakati akitoa elimu kwa Wauzaji na wasambazaji wa gesi za kupikia majumbani semina iliyoandaliwa na kampuni ya taifa Gesi na kufanyika jijini Arusha.
Amesema kuwa ni kosa la kisheria wauzaji kuuza gesi bila kuwa na mizani hivyo wanapaswa kuhakikisha wanakuwa na mizani ili kuepuka hatua Kali za kisheria kwa wale watakaobainika kutokuwa na mizani hizo.
Aidha amedai kwa sasa bado wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao wanauza mitungi ya gesi bila kupima jambo ambalo ni kinyume na sheria kwani uzito unatakiwa kuonekana kabla ya mtumiaji kufikisha nyumbani na kuanza matumizi.
"Mwananchi unatakiwa kuhakikisha kuwa umeona muuzaji akiwa amepima na umejiridhisha kabisa kuwa ni kiwango hicho lakini Kama ni pungufu basi pia utaona", aliongeza Meneja huyo.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara wa uuzaji wa mitungi hiyo ya gesi wakifuata sheria basi changamoto hizo za changamoto za ujazo hafifu zitaisha kabisa kwa wananchi.
aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha kuwa wanakuwa waaminifu na kuachana na tabia ya kupunguza gesi kwani endapo watakamatwa sheria itawafikisha mahakamani.
"Tulifanya msako Moshi na tumeshawafikisha mahakamani wafanyabiashara wawili niwaombe tu ninyi wafanyabiashara wanaofanya hivyo waache kwani ni hatari sana ndani ya jamii", aliongeza.
Naye Bw Joseph Nzumbi ambaye ni meneja mauzo wa Taifa Gesi alisema kuwa bado kwa mikoa ya Kaskazini kuna changamoto ya ujazaji wa mitungi ambayo imejazwa mitaani bila kufuata taratibu hivyo kuwa na hatari kwa watumiaji .
Amewataka wananchi kuangalia ujazo na kifuniko cha juu ambacho hakijafunguliwa pindi wanaponunua gesi ili kuweza kubaini gesi ambazo hazijachakachuliwa.
Social Plugin