AFISA Vipimo Mwandamizi Mkoa wa Simiyu James Kazoba akiwaonesha waandishi wa Habari (hawapo pichani) mzani wa kidijitali utakaoutumika kununulia pamba 2022/23
****
Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
SERIKALI Mkoani Simiyu imesema katika msimu wa 2022/23, Zao la Pamba litanunuliwa kwa utofauti na mikoa mingine kutokana na mkoa huo kuwa kinara wa pamba kwa kuzalisha asilimia 60 ya pamba yote nchini.
Katika msimu huu, pamba itanunuliwa kwa soko huria badala ya kutumia mfumo wa ushirika kama ilivyo kwa mikoa mingine na kwamba wanunuzi watanunua kwa kutumia mawakala au kutumia vyama vya ushirika.
Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Mkoa huo David Kafulila wakati akifungua semina ya siku moja kwa waandishi wa Habari pamoja na Kamati ya Siasa ya mkoa huo kwa lengo la kuweka uelewa wa pamoja.
Kafulila amesema katika msimu wa ununuzi wa Pamba mwaka huu (2022/23) utakuwa na utofauti na mikoa mingine kutokana na matokeo ya uzalishaji wa pamba.
‘’Viongozi, Bodi ya Pamba (TCB) tumependekeza mfumo wa ununuzi wa Pamba kuwa tofauti na mikoa mingine kwa sababu ni kinara wa uzalishaji…kupitia ushirika kulionekana kuna nafasi (gap) kati ya ushirika na mkulima’’ amesema Kafulila, na kuongeza.
‘’Wanahabari tusaidieni, wakulima hawaoni umuhimu wa ushirika kama una msaada kwao, Amcos hazikidhi matarajio ya wakulima…wanahabari muibue ili tuwajibishane’’
Kafulila amewataka viongozi wa ngazi za mkoa, wilaya, kata, vijiji na vitongoji kusimama ili kumsaidia mkulima ambaye amekuwa akiibiwa wakati wa mauzo ya pamba.
Kafulila pia amewataka waandishi wa habari kuandika habari za uchunguzi pamoja na kufuatilia nyendo za pamba zitakazokuwa na tija ambazo zitawafanya viongozi kuwajibika kwa wananchi.
Mtaalamu Mshauri wa Masuala ya Pamba Joshua Mirumbe amesema Mkoa wa Simiyu umepewa mfumo (model) mpya wa ununuzi wa pamba pamoja na wilaya za Magu na Kwimba mkoani Mwanza.
‘’Katika Vituo vya kununulia pamba, eneo liko chini ya Amcos, wanunuzi watakuwa na mawakala wake…kutakuwa na mlango wa ushirika na mlango binafsi ili kuongeza uwazi na ushindani’’ amesema Mirumbe.
Amesema Serikali imeelekeza Ushirika uwepo kwa ajili ya kusimamia, lakini pawepo na milango mingi kwa ajili ya kununuliza zao la pamba, pia kila siku mizani itakuwa inakaguliwa.
Afisa Vipimo Mwandamizi mkoa wa Simiyu James Kazoba amesema katika mkoa wa Simiyu wamekagua mizani 638 na zoezi hilo linaendelea ikiwemo kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mizani.
Sitta Tuma, Mwandishi wa EATV amepongeza kutolewa kwa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ili yawajengee uwezo kwa kuripoti na kuandika habari za pamba kwa usahihi.
May 20, 2022, Serikali kupitia wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba (TCB) ilitangaza kuanza rasmi kwa msimu wa ununuzi wa Pamba mwaka 2022/2023 ambapo pamba itauzwa na kununuliwa shilingi 1560 kwa kilo moja.
Social Plugin