Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WADAU TITYE - KASULU WATUMIA KONGAMANO LA TGNP KUELEZA NJIA ZA KUPUNGUZA VIPIGO, MANYANYASO KWA WANAWAKE


Mratibu wa vituo vya taarifa na maarifa vinavyosimamiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Flora Ndabaniye akizungumza katika kongamano na wadau wa kupinga ukatili katika kijiji cha Titye wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma. 


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

WADAU wa kupinga ukatili wilayani Kasulu mkoani Kigoma wamesema kuwa kujengewa uwezo wa kiuchumi kwa wanawake na kuwafanya kuwa na miradi ya kiuchumi kutapunguza vipigo na manyanyaso wanayopata kutoka kwa waume zao.


Hayo yamebainishwa kwenye kongamano la utoaji elimu na uhamasishaji jamii kupinga ukatili wa kijinsia lililoandaliwa na mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) kwenye kijiji cha Titye wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.


Mmoja wa wananchi waliohudhuria mkutano huo, Esther Martin mkazi wa kijiji cha Titye wilaya ya Kasulu alisema kuwa iwapo wanawake watakuwa na miradi ya kiuchumi ya kuwaingizia kipato kwa kiasi kikubwa inachangia kuwafanya wanaume washindwe kuwafukuza wake zao maana hiyo inaweza kuwarudisha nyuma kiuchumi hata wao.

Alisema kuwa wanaume wengi wanawanyanyasa wanawake wasio na nguvu za kiuchumi kwa kuwaona tegemezi na mzigo kwao hivyo kuwaona hawana mchango kwenye suala la kuhudumia familia tofauti na wanawake wenye miradi ambao wanasaidia kuhudumia familia.

Alibainisha kwamba hata unapotokea mgogoro na wakatengana mwanamke anaweza kuhudumia mahitaji muhimu ya familia ikiwemo mahitaji ya kibinadamu na shule kwa watoto na hivyo kuondoa mateso kwa wanawake na watoto hao.

Mwenyeiti wa kituo cha taarifa na maarifa, Hajira Ramadhani alisema kuwa wamekuwa wakipokea malalamiko na manyanyaso ya wanawake kupigwa na kunyanyaswa na waume zao kwa sababu wanaonekana ni mzigo na hawana msaada kiuchumi kwa familia.


Hajira alisema kuwa wameona kuwa ni lazima wasisitize serikali isimamie mchakato wa mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia halmashauri kwa mapato yake ya ndani ambapo wanawake, vijana na walemavu waweze kupata mikopo na kuendesha miradi ya kiuchumi.

Afisa Maendeleo ya jamii Halmshauri ya wilaya Kasulu, Maria Tarimo alisema kuwa ni ukweli usiopingika kwamba kuwajengea uwezo wa kiuchumi wanawake kunapunguza ukatili na unyanyasaji kwa wanawake na kujenga imani kwa wanaume kuwashirikisha wake zao kwenye maamuzi mbalimbali.


Tarimo alisema kuwa ili kufikia hatua hiyo halmashauri kupitia idara ya maendeleo ya jamii imekuwa ikiendesha mipango ya kuunda vikundi kwa wanawake ili kuwezesha upatikanaji rahisi wa mikopo itakayowezesha kuendesha miradi ya kiuchumi.

Mratibu wa vituo wa taarifa na maarifa vinavyosimamiwa na Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP), Flora Ndabaniye alisema kuwa moja ya majukumu ya vituo hivyo ni kufikisha taarifa na maarifa kwa wananchi jinsi ya kukabili ukatili na unyanyasaji kijinsia kwa wananchi wanoishi kwenye maeneo hayo.


Ndabaniye alisema kuwa ukatili wa kijinsia unaweza kupigwa vita na kutoweka iwapo jamii itashirikiana kupambana na hali hiyo kwani mambo hayo yanatokea kwenye jamii yenyewe ambapo alisema kuwa uzoefu uliotolewa wa kuwajengea uwezo wa kiuchumi wanawake ili kuepukana na ukatili wa vipigo na manyanyaso kwa wanawake hauna budi kusimamiwa na kutekelezwa na wanajamii wenyewe kwa karibu.
Mratibu wa vituo vya taarifa na maarifa vinavyosimamiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Flora Ndabaniye akizungumza katika kongamano na wadau wa kupinga ukatili katika kijiji cha Titye wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma. Picha na Fadhili Abdallah
Ebeno Fabiano Mkazi wa kijiji cha Titye wilaya ya Kasulu akizungumza katika kongamano la kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia lililoandaliwa na mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) yenye lengo la kujenga uelewa kwa jamii kujitokeza kupinga vitendo vya unyanyasaji kijinsia lakini kuwaripoti watu wanaofanya vitendo hivyo.
Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Titye wilaya ya Kasulu mkoa Kigoma akitoa maoni yake wakati wa kongamano la kupinga ukatili na unyanyasaji kijinsia lililoandaliwa na Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP)
Mwenyekiti wa kituo cha taarifa na Maarifa kijiji cha Titye wailaya ya Kasulu mkoani Kigoma Hajiri Ramadhani akizungumza kwenye kongamano la kupinga ukatili na unyanyasaji kijinsia lililoandaliwa na mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) yenye lengo la kujenga uelewa kwa jamii kujitokeza kupinga vitendo vya unyanyasaji kijinsia lakini kuwaripoti watu wanaofanya vitendo hivyo.
Wananchi na viongozi wa kijiji cha Titye wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wakiwa kwenye vikundi vya majadiliano kuweka maazimio ya hatua za kuchukua kukabiliana na tatizo la ukatili wa kijinsia hapa walikuwa kwenye kongamano la kupinga ukatili wa kijinsia lililoandaliwa na Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) kijijini hapo.
Wananchi na viongozi wa kijiji cha Titye wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wakiwa kwenye vikundi vya majadiliano kuweka maazimio ya hatua za kuchukua kukabiliana na tatizo la ukatili wa kijinsia hapa walikuwa kwenye kongamano la kupinga ukatili wa kijinsia lililoandaliwa na Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) kijijini hapo.
Picha na Fadhili Abdallah

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com