Mwanaume jijini Nairobi nchini Kenya aliyetambulika kama Alex Omondi amevuma sana kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuwasihi maofisa wa polisi kumtia mbaroni, kwa sababu alikosa mahali pa kulala.
Mwanaume huyo aliyeonekana kufikishwa ukingoni na ugumu wa maisha, baada ya kukosa mahala pa kujilaza usiku wa giza, aliona ni heri alale kwenye kituo cha polisi.
"Sina mahala pa kulala. Nyumba ninakoishi imefungwa na 'landlord'. Sasa niko hapa kwa sababu kauli mbiu ya polisi ni utumishi kwa wote," mwanaume huyo alianza kujielezea.
Wakati polisi walipomuuliza ni usaidizi wa aina gani alitaka apewe, mwanaume huyo alipendekeza atupwe korokoroni.
Omondi aliwaambia polisi hao kwamba ni wao wataamua ikiwa wanataka kumuachilia huru ifikapo asubuhi, au wamlimbikizie makosa ili apelekwe kortini.
Alijilazimisha kufanya kosa mbele ya polisi ili wamkamate
Ikizingatiwa kwamba mwanaume huyo hakuwa na hatia, polisi hao walikuwa na wakati mgumu kufanya alichotaka.
Wakati polisi hao waliposisitiza kuwa sio kazi yao kuwakamata raia wasiokuwa na hatia, Omondi aliomba mahala pa kuketi.
"Au niende nishukishe ile bendera ndipo mpate sababu ya kunitia mbaroni?" mwanaume huyo alizidi kuwasumbua polisi.
Haijabainika iwapo polisi walisikia kilio chake au la, ila ni muhimu kwa mwanaume huyo kupata usaidizi ili asikate tamaa maishani.
Chanzo- Tuko news