WAKATI Serikali ikiendelea na uzinduzi wa Filamu ya Royal Tour,aliyoshiriki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan,kutangaza utalii nchini,aliyekuwa Mbunge wa Kahama mwaka 2005 hadi 2015,James Lembeli,ameibuka na kutoa ushauri.
Lembeli ambaye katika kipindi chake cha Ubunge alipata kuhudumu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na Mazingira,alisema Filamu hiyo ingependeza kuzinduliwa huku kukiwa na mkakati endelevu wa kuikuza sekta hiyo kwa kufungua Ofisi za Bodi ya Utalii ( TTB )katika nchi zenye kuleta watalii wengi Nchini.
Alizitaja nchi ambazo zitastahili kufunguliwa ofisi hizo kuwa ni ,Ujerumani,Marekani,Uingereza,China na Ufaransa,kama ambavyo nchi za Afrika Kusini,Rwanda,Kenya na Zimbabwe zilizofanya,hivyo kusaidia ushindani katika sekta ya utalii duniani.
Pia alishauri kuwepo umuhimu wa kutenga bajeti ya fedha za kutosha kwa ajili ya Bodi ya Utalii zitakazowezesha kuziendesha ofisi katika nchi hizo na kuondokana na kasumba ya kutegemea ofisi za Ubalozi zenye majukumu ya kidiplomasia kutekeleza majukumu hayo.
Alifafanua kuwa Maafisa wa Ubalozi kwa asilimia kubwa hawana taaluma ya uhifadhi na utalii,jambo ambalo kwa mara kadhaa wamejikuta wakitoa taarifa zisizo sahihi pindi watu wanapofika ubalozini kupata taarifa za vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.
“Kadhia hii ilipata kutokea mwaka 2003, nikiwa miongoni mwa maafisa wa Wizara ya Maliasili Utalii katika maonyesho ya Berlin, Ujerumani.Wakala mmoja mkubwa wa utalii nchini humo alilalamika kutopewa taarifa sahihi za idadi kamili ya Faru walioko Ngorongoro",alisema Lembeli.
Aliendelea kusema, “wakala huyo aliambiwa na maafisa wa ubalozi wako faru 300 ,na wageni walipofika Ngorongoro walibaini kwamba wamedanganywa hivyo kutaka kumshitaki kwa uongo na udanganyifu.”
Alibainisha watendaji wengi wa serikali kuu na katika balozi zetu,hawajawahi kufika katika hifadhi zetu na hata Zanzibar,hivyo kuhoji wanawezaje kutoa taarifa sahihi za maeneo hayo huku taarifa walizonazo wakisoma kwenye vitabu,majarida,vipeperushi au kuona katika “Safari Chanel”.
Lembeli aliyepata kuhudumu Hifadhi ya Taifa,akiwa Meneja Mawasiliano kwa zaidi ya miaka 15,kupitia taaluma yake ya uandishi wa habari,akihamasisha na kuitangaza Tanzania duniani,alipongeza hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan,na kudai pasipo mikakati thabiti haitokuwa na tija
Alionesha khofu yake pasipo mkakati maalumu filamu hiyo,kuishia katika kabati za kutunza nyaraka za serikali,hivyo kumuomba Rais Samia kuhakikisha inasimamiwa kikamilifu na serikali na Taasisi husika kwa kuona Filamu ya Royal Tour ikiendelea kutangazwa duniani kote.
Lembeli alijinasibu kufanya kazi iliyotukuka ya kuutangaza utalii akiwa na Waziri wa Maliasili wa wakati huo,Zakhia Hamdani Meghji,na kupongeza hatua ya Rais Samia juu ya hatua ya filamu hiyo ambayo imeanza kuleta tija nchini.
Aidha aliifananisha filamu ya Royal Tour na inayoitwa Serengeti haitakufa ( Serengeti shall never die) iliyotengenezwa mwaka 1956 na Mjerumani,Michael Girmick,ambayo kwa kipindi cha miaka 65 tangu kutengenezwa ikiendelea kutangaza maajabu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na Tanzania,duniani.
Aliendelea kusema kuwa filamu hiyo ya Serengeti Shall Never Die haitakufa imeendelea kudumu miaka yote 65 kutokana na serikali ya Ujerumani kupitia Taasisi ya Frankfurt Zoological Society kila mwaka kutenga fedha ya kutosha kuhakikisha filamu hiyo inatangazwa na kuongeza watalii katika nchi yetu.
Aidha alibainisha kama ilivyo kwa filamu hiyo ya Serengeti, Royal Tour itadumu kuwa nyenzo muhimu kwa kuitangaza Tanzania duniani kwa miaka 100 ijayo huku akitaka Wanaobeza kazi na uamuzi uliofanywa na Rais Samia,kuelimishwa.
Alisema watu hao hawaijui tasnia ya utalii sambamba na kutofahamu gharama na jasho linalotumika na serikali za nchi na wadau,hasa wafanyabiashara wa sekta hiyo kuleta watalii nchini,hivyo kueleimishwa kutasaidia kuona umuhimu wa filamu hiyo kwa Taifa.
Social Plugin