Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imepunguza tozo kwa asilimia 30 kwa Bandari ya Tanga na Mtwara ikiwa ni mikakati ya kuhakikisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi wanatumia bandari nchini.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo bungeni alipokuwa swali la Mbunge wa Nanyamba(CCM), Abdallah Chikota kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo.
Chikota katika swali lake, amehoji serikali ina mkakati gani kuhakikisha wafanyabiashara wa Sudan na Uganda kwa upande wa Tanga na Mtwara nchi za Kongo, Malawi na Zambia wanatumia bandari ya Tanga.
Majaliwa akijibu swali hilo, amesema hatua hiyo ya kupunguza tozo inatokana bandari nyingi za pembezoni zimekuwa hazina wateja wengi kama ilivyo bandari ya Dar es Salaam.
Amesema lengo ni kuwavutia wafanyabiashara hususani nchi za jirani kutumia bandari zilizo karibu na nchi hizo na kutolea mfano Bandari ya Mtwara kutumiwa zaidi na nchi za Malawi na Msumbiji.
“Serikali imekuwa ikiboresha na kuimarisha mita za mafuta katika bandari mbalimbali na sasa inakaribisha meli za mafuta kushusha pia mafuta katika bandari za Mtwara na Tanga. Mamlaka ya bandari pia inatumia balozi zetu kuhamasisha wafanyabiashara wa huko kutumia bandari zetu na tumefungua ofisi Kongo, Malawi, Uganda ili zitumike kurahisisha mawasiliano,” ameeleza.
Kadhalika, amesema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya maboresho ya bandari zote nchini zilizopo ukanda wa bahari kuu na maziwa makuu ikiwamo kuimarisha miundombinu na huduma mbalimbali.
“Pia mikakati ya serikali ni kuvutia matumizi ya bandari zote nchini inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuongeza vifaa vya kupakua na kupakia mizigo kwa muda mfupi ili matumizi ya bandari yawe ya muda mfupi na pia imepunguza tozo hasa kwa bandari ya Tanga ili kuvutia wafanyabiashara,”amesema.
Social Plugin