Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAVIKUMBUKA VITUO VYA WALIMU 'TRC' KWA KUBORESHA MIUNDOMBINU NA KUVIPA VITENDEA KAZI

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha Seleman Msumi akikabidhi vitendea kazi hivyo kwa waratibu elimu


Rose Jackson,Arusha

Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu, kupitia Wizara ya Elimu, imevikumbuka vituo vya walimu 'Teacher's Resources Center (TRC)', kwa kuanza kuboresha miundombinu na kuvipa vitendea kazi.

Wizara hiyo ya Elimu, imetoa seti tano za mashine za kudurufia karatasi kwa vituo vitano vya walimu, halmashauri ya Arusha, lengo likiwa ni kuviwezesha vituo hivyo, kuanza kufanya kazi upya, kwa ajili ya kuwaendleeza walimu kitaaluma wawapo kazini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mashine hizo, mkurugenzi Mtendaji, halmasahuri ya Arusha, Seleman Msumi, amethibitisha kupokea seti tano za mashine na wino, kutoka Wizara ya Elimu, kwa ajili ya kutumiwa na vituo vitano vya TRC vya halmashauri hiyo.

Mkurugenzi Msumi, amesema serikali katika kuboresha sekta ya elimu, inajikita pia katika kuboresha mazingira bora kwa kuwapa walimu fursa ya kupata mafunzo kazini, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo katika stadi za ujifunzaji na ufundishaji unaoendana na mabadiliko ya kiteknolojia.

"Kazi ya kufundisha inatakiwa kujifunza mara kwa mara, serikali kupitia vituo vya TRC, imeona umuhimu wa kuvihuisha vituo hivyo, ili walimu waweze kupata mafunzo kazini wakati wote, hivyo niwatake walimu kutumia fursa hiyo adhimu kwa kujinoa kitaaluma, pamoja na kubadilishana uzoefu wa mbinu za ufundishaji na ujifunzaji, unaoendana na wakati na mabadiliko ya kiteknolojia", amesisitiza Mkurugenzi Msumi.

Naye Kaimu Afisa Elimu Msingi, Ruth Sumari, amefafanua kuwa, lengo la serikali kutoa vifaa kwenye vituo vya TRC, ni kuhakikisha walimu wanapata elimu wakiwa kazini, inayowajengea uwezo wa kuendeleza mbinu mbalimbali za ufundishaji ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza stadi tatu za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu, maarufu kama KK tatu.

Amefafanua kuwa, halmashauri ina jumla ya vituo vitano vya TRC, na kuvitaja vituo hivyo ni pamoja na Kiutu, Mlangarini, Mateves, Oloirien na Lengijave, vituo ambavyo vitahudumia shule zote 132 za serikali za msingi na sekondari za halmashauri.

Hata hivyo, Wasimamizi wa vituo hivyo vya TRC, halmashuri ya Arusha, licha ya kuishukuru na kuipongeza serikali ya awamu ya sita, kwa kuvihuisha vituo vya TRC, wameweka wazi kuwa vituo hivyo ni muhimu kwa walimu kwa kuwa vinawapa fursa ya kupata mafunzo, mafunzo ambayo yanawezesha walimu kujifunza na kufundisha, kunako endana na wakati, na kuahidi kutumia vituo hivyo kwa maendeleo ya walimu na kupandisha kiwango cha taaluma kwa wanafunzi.

Msimamizi wa TRC Kiutu, na Mratibu wa Elimu kata ya Kiutu, Mwalimu Evaline Mosha, amesema kuwa, TRC ni muhimu sana kwa walimu, kwa kuwa ni kituo kinachowakutanisha walimu kujiendeleza kitaaluma, kwa kujifunza moduli mbalimbali za ualimu zinatolewa na wizara, pamoja na kubadilishana uzoefu katika nyanja za ufundishaji na ujifunzaji wawapo kazini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com