Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka (kulia), akipata maelezo mafupi kutoka kwa Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof. Emmanuel Luoga ( wa pili kutoka kulia), kuhusu Kiti cha utafiti cha O.R.Tambo alipowasili katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kwa ajili ya uzinduzi wa Kiti cha Utafiti cha O.R. Tambo jijini Arusha
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof Eliamani Sedoyeka, akisikiliza taarifa kuhusu uzinduzi wa Kiti cha Utafiti Cha O.R Tambo wakati wa hafla hiyo Katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela
Mwenyekiti wa kiti Cha Utafiti Cha O.R Tambo Prof. Hulda Shahidi Swai (Kushoto) akifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof Eliamani Sedoyeka(hayupo pichani) wakati wa Uzindizi wa Kiti hicho tarehe 18 Mei, 2022 kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa UNESCO Prof. Hamisi Malebo.
Meneja wa Kiti cha Utafiti Cha O.R Tambo katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Ndg. Victor Jape (kushoto) akisikiliza hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof Eliamani Sedoyeka ( hayupo pichani) wakati wa Uzindizi wa Kiti hicho tarehe 18 Mei, 2022 kulia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dodoma Dkt. Rehema Kilonzo.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kikao Cha uzinduzi wa kiti Cha Utafiti Cha O.R Tambo katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela tarehe 18 Mei, 2022 kushoto kwake ni Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Emmanuel Luoga na wa kwanza kulia kwake ni Mwenyekiti wa kiti Cha Utafiti Cha O.R Tambo Prof. Hulda Shahidi Swai.
.................................................
Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela imezindua Kiti cha Utafiti cha O.R. Tambo jijini Arusha.
Kiti hicho kitajikita kwenye utafiti wa malaria na kilimo kwa kuchagiza matumizi ya teknolojia katika upatikanaji wa dawa za kutibu malaria zenye uwezo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na pia kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa husika kwa mgonjwa. Aidha, utafiti pia utajikita kwenye kilimo kwa kuleta mbolea na viuatilifu vinavyofanya kazi kwa ufanisi zaidi kwenye mazao na kupunguza athari za kimazingira kwenye ardhi.
Akizungumza katika uzinduzi wa Kiti hicho cha Utafiti cha O.R. Tambo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Eliamani Sedoyeka amesema kuwa uzinduzi wa kiti cha utafiti cha O.R. Tambo Afrika ni chachu katika kuongeza ufanisi wa madawa ya malaria na viatilifu vya kilimo nchini.
“Sote tunafahamu kuwa malaria bado ni changamoto kubwa nchini ambao unaathiri uchumi kwa kupunguza nguvu kazi ya taifa kutokana na kupoteza maisha ya watanzania wengi” amesema Profesa Sedoyeka.
Ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuagiza mbolea na viwatilifu ambavyo nyingi hazina ufanisi na zina athari kwenye mazingira, hivyo utafiti na uzalishaji nchini wa mbolea na viwatilifu venye ufanisi zaidi na zisizoathiri mazingira utasaidia nchi yetu kupunguza gharama za kuagiza bidhaa hizo na pia kuongeza mavuno kwa wakulima na kuboresha mazingira kwa kupunguza kemikali zenye sumu kwenye ardhi na hewani.
Akizungumzia faida za kiti cha utafiti cha O.R. Tambo, Mwenyekiti wa O.R. Tambo, Prof. Hulda Shaidi Swai amesema kuwa pamoja na kuimarisha ufanisi wa dawa za kupambana na malaria, mbolea na viwatilifu venye tija zaidi kiti hiki pia kitatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa shahada za uzamivu na uzamili na hivyo kuongeza idadi ya wanasayansi nchini.
Naye Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Profesa Emmanuel Luoga amesema kuwa Pamoja na mabo mengine, Kiti cha O.R. Tambo kitasaidia kuboresha maabara ya Taasisi ya Nelson Mandela hivyo kutengeneza mazingira rafiki kwa wanafunzi kufanya tafiti zao.
Kiti cha Utafiti cha O.R. Tambo kimefadhiliwa kupitia ushirikiano kati ya Mfuko wa Taifa wa Utafiti wa Afrika Kusini (NRF) na Idara ya Sayansi na Ubunifu (DSI), Taasisi ya Oliver na Adelaide Tambo, Kituo cha Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa cha Canada (IDRC), na Halmashauri saba za Mpango wa Mabaraza ya Utoaji wa usaidizi wa Sayansi Kusini mwa Jangwa la Sahara (SGCI).
Mradi huo unatekelezwa kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH).
Imeandikwa na Orester Julius, Afisa habari wa Kituo cha Umahiri cha CREATES –NFS NM- AIST
Social Plugin