Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari akiongoza kikao-kazi na watoa huduma za Mawasiliano katika Kanda ya Ziwa, kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tarehe 24 Mei, 2022 kujadili utendaji kazi na kusikiliza changamoto zinazoikabili sekta ya mawasiliano katika kanda ya ziwa ili kuzipatia ufumbuzi. Washiriki kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Shinyanga, Geita, Mara na Simiyu wameshiriki kikao hicho. Picha na TCRA
Baadhi ya watoa huduma za Mawasiliano katika Kanda ya Ziwa wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dkt. Jabiri Bakari akiongoza kikao-kazi na watoa huduma katika kanda hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tarehe 24 Mei, 2022, kujadili utendaji kazi na kusikiliza changamoto zinazoikabili sekta ya mawasiliano katika kanda ili kuzipatia ufumbuzi. Washiriki kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Shinyanga, Geita, Mara na Simiyu wameshiriki kikao hicho. Picha na TCRA
Watoa huduma za mawasiliano katika Kanda ya Ziwa wakishiriki kikao kazi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kilichoongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Jabiri Bakari na kufanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tarehe 24 Mei, 2022. Kikao hicho kililenga kujadili utendaji kazi wa watoa huduma katika kanda hiyo ambapo TCRA ilisikiliza na kupokea changamoto zinazoikabili sekta ya mawasiliano katika kanda ili kuzipatia ufumbuzi. Washiriki kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Shinyanga, Geita, Mara na Simiyu wameshiriki kikao hicho. Watoa Huduma za Utangazaji kwa njia ya Redio, Televisheni na Mitandao, Televisheni za Kebo, Watoa Huduma za Mawasiliano ya Simu, Wamiliki wa Kampuni za Usafirishaji wa Vifurushi na Vipeto, Watoa Huduma za Intaneti pamoja na Umoja wa Mafundi Simu Kanda ya Ziwa. Picha na TCRA
*********************
° Changamoto za Watoa Huduma Zatafutiwa Mwarobaini
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeweka bayana dhamira yake kuboresha sekta ya mawasiliano nchini kwa kuhakikisha watoa huduma za mawasiliano wanazingatia kutoa huduma za mawasiliano zenye ubora na ufanisi.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt Jabiri Bakari katika kikao kazi na wadau wa sekta ya mawasiliano Kanda ya Ziwa kufanya kupokea hoja mbalimbali na maoni ili kuboresha sekta ya mawasiliano nchini.
Kikao kazi hicho kilihusisha watoa huduma za utangazaji kwa njia ya redio, televisheni na mitandao, televisheni za kebo, watoa huduma za mawasiliano ya simu, wamiliki wa kampuni za usafirishaji wa vifurushi na vipeto, watoa huduma za intaneti pamoja na umoja wa mafundi simu kanda ya ziwa na kufanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari akiambatana na Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo na Meneja wa Sehemu ya Masuala ya Wateja TCRA Bw. Thadayo Ringo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu usalama mtandaoni, Mkurugenzi Mkuu Jabiri alisisitiza kuwa, TCRA kwa kushirikiana na wadau wengine wa usalama mtandaoni itaendelea kuhakikisha inatoa ushirikiano stahiki kwa Vyombo vinavyolinda usalama wa watumiaji huduma za mawasiliano nchini, ili watumiaji wajisikie huru kutumia huduma hizo pasipo wasiwasi wa usalama wao wakati wote wanapokuwa kwenye mazingira ya mtandaoni.
“Mbinu za wahalifu pia zimebadilika, kutoka kwenye kutenda uhalifu katika mazingira ya kawaida, sasa wahalifu wamehamia mtandaoni; kwa hiyo jinsi inavyoendelea na sisi lazima tuendelee na kujiongeza. Tulitoa maelekezo watoa huduma za mawasiliano ya simu lazima wawasiliane na wateja wao kwa kutumia namba 100 kwa hiyo ukipata taarifa ya simu namba nyingine na ukakubaliana maana yake kuna tatizo” alisisitiza Jabiri na kuongeza kuwa TCRA inashirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha mazingira ya mawasiliano kwenye mtandao yanaendelea kusalia salama kwa kila mtumiaji wa huduma za mawasiliano.
“Wahalifu wanavyobadilika na sisi tunabadilika; kwa hiyo niseme tuna kazi kwenye hilo eneo, huu ni uhalifu kama uhalifu mwingine kwa hiyo taarifa za uhalifu kwenye mtandao zinapaswa kwenda kwenye Kituo cha Polisi; Polisi wana Kitengo cha kushughulikia uhalifu mtandaoni, nasi tumeendelea kushirikiana nao, ili kushughulikia na kudhibiti uhalifu wa aina hii kama wanavyoshughulikia uhalifu wa namna nyingine” alisisitiza Jabiri akijibu baadhi ya hoja za washiriki wa kikao hicho waliotaka kupata ufafanuzi wa namna Mamlaka hiyo inavyodhibiti uhalifu mtandaoni.
Kuhusu faragha ya taarifa za mtumiaji wa huduma za mtandao, Mkurugenzi Mkuu Jabiri alibainisha kuwa, usalama wa taarifa za mtumiaji wa huduma za mtandao unalindwa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa Mtandaoni, hata hivyo mchakato wa sheria kamili itakayolinda faragha za mtumiaji wa huduma za mawasiliano unaendelea na Matarajio na kwa sheria hiyo kuanza kutumika hivi karibuni, alisisitiza Jabiri na kuongeza; “Watoa huduma ambao wanabeba taarifa za watu (personal data), wanawajibika kwa namna moja au nyingine kuhakikisha kwamba faragha ya mtumiaji wa huduma zao inalindwa, wakati hii sheria haijafika, sheria ya Uhalifu Mtandaoni haijawaacha pia; na ndiyo maana falsafa tuliyonayo hivi sasa ni kuhakikisha tunaongeza jitihada za Ufuatiliaji kwa watoa huduma wetu wote” alisisitiza Jabiri.
Aidha, Jabiri aliwaeleza wadau hao kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inaandaa kituo cha taarifa cha kimtandao ‘portal’ kiitwacho Tanzanite mahali ambapo watoa huduma za mawasiliano na wadau watapata taarifa mbalimbali zinazohusu sekta ya mawasiliano.
“Ninyi watoa huduma ndiyo wateja wetu, lakini na ninyi watoa huduma mnao wateja mnaowahudumia, kwa hiyo tumeboresha huduma kwa kuweka mazingira wezeshi; tumeweka fursa ambayo sasa unaweza kupata fursa ya kujadiliana masuala ya sekta na wahandisi, wanasheria, na wachumi wakakushauri zaidi jinsi ya kuboresha na kupanua huduma unazotoa na kuongeza tija ili kuwahudumia wananchi katika sekta pana ya mawasiliano. Tumeboresha dawati hili la huduma kwa mteja lipo ofisi za Makao makuu na tutalifikisha kwenye ofisi zetu za kanda” alibainisha Jabiri.
Katika kikao-kazi hicho TCRA imepokea hoja katika masuala ya Leseni za Mawasiliano, usafirishaji vifurushi na vipeto, masuala ya vifurushi vya mawasiliano ya simu, huduma za utangazaji na posta na kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo ya wadau wa sekta kama yalivyopokelewa kutoka kanda ya ziwa; ambapo Mkurugenzi Mkuu Jabiri alisisitiza kuwa lengo la kikao hicho kama ilivyo kwa vikao vingine ni kuboresha sekta ya mawasiliano Tanzania.
Social Plugin