Moja ya majengo yanayovutia katika mji wa kisasa wa Serikali uliopo eneo la Mtumba,Jijini Dodoma.
Hayati John Pombe Mgufuli,Rais wa awamu ya tano wa Tanzania ambaye pia ni muasisi wa Mji wa Serikali-Mtumba.
Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog-DODOMA.
Ni miaka mitano sasa tangu Serikali ilipoamua kuhamishia makao yake makuu Dodoma ikitokea Jijini Dar Es Salaam baada ya aliyekuwa Rais wa Tanzania , John Pombe Magufuli kutangaza rasmi kuhamia katika jiji hili akiwa ni Rais wa kwanza kati ya marais watano waliotangulia kutekeleza uhamisho wa makao makuu ambao umechukua safari ya zaidi ya miaka 45 iliyopita.
Rais Magufuli alitoa amri ya
serikali kuhamia Dodoma mwezi Julai 2016 wakati alipopewa wadhifa wa mwenyekiti
wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi.
ambapo Waziri mkuu alianza kuhamia katika mji huu na kufuatia na viongozi wengine pamoja na wizara tangu mwaka 2016.
Jambo hili lilitazamwa kama fursa kwa watanzania na hasa wenyeji wa mkoa wa Dodoma”wanyausi” katika mageuzi ya kiuchumi hasa kwa mtu mmoja mmoja kutokana na kuwepo kwa uwazi wa shughuli mbalimbali za uchumi zinazotokana na ujenzi wa Mji wa kiserikali unaofahamika kama ‘MJI WA MAGUFULI’wenye fursa kwa mama lishe(ntilie),wajenzi,biashara nk.
Lakini kwa wenyeji wa Dodoma ambao kwa lugha nyingine huitwa 'wanyausi' limekuwa tofauti ambapo baadhi yao waneshindwa kuingia kwenye fursa hii na badala yake wamejiingiza katika ulevi kupindukia kiasi kinachopelekea kudhoofu na kuwa nyuma kimaendeleo.
Tumeshuhudia vijana wengi ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa kwa huko vijijini wanapoteza uelekeo kwa kutumia muda mwingi kustarehe katika vilabu vya pombe hata katika muda waliopaswa kuutumia kufanya kazi.
Kwa ujumla jambo hili linawakera baadhi ya wenyeji wa mkoa huu ambao ni wagogo na kuamua kulikemea kwamba huenda likaleta ahueni na kuwapa hadhi .
Licha ya kuwepo kwa kaulimbiu nyingi za viongozi wa juu zinazohamasisha watu kufanya kazi kwa bidii ikiwemo ile ya Hayati Magufuli”HAPA KAZI TU”na hii ya sasa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan “KAZI IENDELEE”bado kuna watu vichwa ngumu hawatilii maanani msisimko huo na kuishia kujibweteka ili mradi siku ziende.
Watu wa aina hii tunaweza kuwaita vichwa ngumu maana hata baada ya kuwepo kwa juhudi nyingi za Serikali ya Mkoa huu kupitia Mkuu wa mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka kuhamasisha watu kutumia muda wa kazi kufanya kazi,mambo bado yako vilevile huku Pombe ya kienyeji na gongo ikiendelea kuwa gumzo kwa watu waishio vijijini kwa kuuzwa masaa 24 bila woga wowote.
Kulingana na sheria iliyopo baa zote zinapaswa kufunguliwa kuanzia mida ya jioni kupisha mida ya kazi kutumika kuimarisha uchumi.
Kijiji cha Mtumba kilichopo Kata ya Mtumba, mahali ulipo mji wa Serikali Jijini hapa ni miongoni mwa vijiji vingi vya Mkoa wa Dodoma ambavyo wenyeji wake (wanyausi)hususani vijana hutumia muda wao mwingi kwenye vijiwe vya pombe na kuona kama ni ufahari.
Kama hiyo haitoshi,ukitembelea kwenye vilabu vya pombe kuanzia asubuhi utakuta vijana wengi wanakunywa pombe huku wakiwa wamelegea Kwa kukosa lishe yaani kazi ni moja kunywa tu bila kupata chakula.
Hata hivyo ni vigumu kuamini kwamba suala hili haliwaumizi hata kidogo Viongozi wa Kijiji hicho,unaweza kujiuliza maswali mengi kwamba inamaana hawaoni kuwa hili ni tatizo au ni kuogopa kuingilia yasiyowahusu?!.
Jambo hili limekuwa gumu mno kwa baadhi ya wazazi wa vijana hao kwani watoto wao ambao wanategemewa kama nguvu kazi ya familia na taifa wanaangamia huku wahusika wa vilabu vya pombe na wauzaji wakijinufaisha.
Hali hiyo imepelekea wazazi wengi kuchoshwa na tabia hiyo huku wakitoa lawama kwa wauzaji wa gongo na kuomba Serikali ya Mkoa wa Dodoma kuingilia kati suala hilo kwa kuwataka wahusika wa pombe hizo kufuata kanuni za uuzaji.
Mariam Wowa mkazi wa Kijiji cha mtumba anasema ,vijana wa kigogo ambao ni Wazawa wa eneo hilo "wanyausi"walipaswa kuwa wanufaika wa kwanza na ujenzi wa mji huo lakini hawana Tena nguvu .
Kutokana na hayo amemwomba Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka na taasisi nyingine za kiraia zinazopinga matumizi mabaya ya pombe kuingilia kati suala hili na kuliangalia kwa jicho la tatu .
"Tumechoka na hali hii,hatuoni hata Serikali ya Kijiji ikikemea aina hii ya ulevi wa kupindukia ,naona sasa tujaribu kuomba msaada kwa Mkuu wetu wa Mkoa atusaidie,imani yangu ni kwamba suala hili lipo ndani ya uwezo wake kwani neno la Mkuu ni amri,"anasisitiza.
Anasema,mara nyingi vijana hao huenda kutafuta vibarua kwenye ujenzi unaoendelea wa Mji wa Serikali na wanapolipwa ujira wao huangukia kwenye ulevi badala ya kufanya maendeleo.
"Tulipoona Serikali inajenga Ofisi zake kijijini hapa tulifurahi ,tukaona tumepata mkombozi kwa kuwa itakuwa ni sehemu ya ajira kwa watoto wetu kufanya kazi pale na watapata fedha kujiendesha kiuchumi,
Cha kushangaza hali imekuwa ndivyo sivyo kwani wanapoenda kufanya kazi ujira wanaopata humalizia kwenye ulevi na mambo mengine ya anasa,naumia sana mimi kama mzazi,"anasema.
Anazidi kueleza kuwa kutokana na kulewa sana vijana hao hujikuta wanadhoofika na kushindwa kuhimili kazi ngumu na hivyo kupelekea vijana wengine awanaotoka mikoa jirani kunufaika na fursa hiyo.
"Hatukatai watanzania wengine kufanya kazi kwenye mji wa Serikali ni jambo jema,lakini inauma kuona vijana wetu hawataki kufanya kazi,wamekuwa wavivu wa kupindukia mpaka wengine wameamua kujiingiza kwenye makundi mabaya ya uporaji na kucheza kamali,"amesema mama huyo.
Naye Janeth Mselemu anaeleza kuwa wakati vijana ambao ni wageni wakizidi kushamiri hali ya vijana wa Dodoma hususani wa pembezoni inazidi kudorora na kuwa na umasikini kiasi kwamba hushindwa hata kukidhi gharama za matibabu na elimu kwa jamii yao.
Kama hiyo haitoshi anafafanua kuwa wenyeji wengi bado wanashindwa kuchangamka kwa kufanya kazi na kupelekea kushindwa hata kumudu gharama za kuwapeleka shule watoto wao.
"Kwa ujumla sisi wazawa hususani wagogo bado hatuna Ari ya maendeleo,tunatakiwa kujifunza Kwa wenzetu,wengine wamekuja tunawaona hawana kitu lakini Sasa Wana viwanja na wengine wamejenga nyumba,tuukatae uvivu kwani ni adui wa ujenzi wa taifa,"anaongea kwa kusikitika
Anaeleza kuwa,vijana wengi wanaofanya kazi Katika ujenzi wa makao ya Serikali ambao wamehamia dodoma Kwa shughuli za kutafuta kipato wamekuwa na maendeleo makubwa ikilinganishwa na Wazawa.
"Naumia Kuona wageni wanaotoka mikoa mingine wanasonga mbele,imedikia wakati vijana wetu wamegeuka kuwa vibarua wao,wanalinda mashamba Yao wakati walipaswa wao ndio wawe wamiliki,lakini hata hawashtuki wanaona sawa tu Ili mradi liende,"anaeleza .
Hata hivyo mama huyo anatumia nafasi hiyo kueleza kuwa wanyausi wanapaswa kujifunza kwa waliofanikiwa na kuacha kubaki nyuma kwani fursa ya makao makuu ni ya watanzania wote.
Suala hili halijaonekana kuwa geni miongoni mwa watu wengi kwani hata wageni wengi wanaoingia Mkoani hapa wakija kusaka fursa hueleza kuwa wanyausi ni wavivu na hawajafunzwa kufanya kazi ndiyo maana wanapitwa na fursa hizi.
Ananieli Mrema mwenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro anaeleza kuwa alikuja Dodoma na kupokelewa na mwenyeji wake ambaye ni mzawa wa Dodoma ambaye alimtafutia connection ya kazi katika mji wa Serikali (Mji wa Magufuli)lakini jambo la kushangaza mwenyeji wake huyo hapendi kabisa kufanya kazi hizo za vibarua.
"Asikwambie mtu,wagogo ni wakarimu Sana lakini linapokuja suala la kufanya kazi hawafanyi kwa malengo wao huangalia leo yao tu hawaoni kesho itakuwaje ,ni wavivu wengi wapo kutafuta pesa ya mlo wa siku moja ,nadhani hii ndo imesababisha ile hulka ya wagogo wengi kuwa ombaomba,"anaeleza huku akiweka mzaha.
Kutokana na hayo Waziri wa mwenye dhamana ya masuala ya Uwekezaji nchini Dkt.Ashatu Kijaji hivi karibuni amemwelekeza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka Kuona haja ya kukaa na vijana wa Mkoa huu kuona namna ya kuawasaidia ili waache uvivu.
Katika ziara yake aliyoifanya katika Kijiji cha Nala kwenye kiwanda kikubwa cha mbolea kinachojengwa na wawekezaji kutoka Burundi iliyolenga kuhamasisha masuala ya uwekezaji ,Dkt.Kijaji alimweleza Mkuu huyo wa Mkoa kutumia nafasi yake kuwaelimisha Vijana namna bora ya kunufaika na fursa zinazojitokeza.
Hatua hiyo ni kutokana na kuelezwa na Mtaka kuwa hata vibarua wanaosaidia ujenzi katika kiwanda hicho cha mbolea wametoka Burundi kwa madai ya kurahisisha ujenzi kumalizika haraka kutokana na vibarua wa Dodoma kukosa sifa.
Katika taarifa yake Mtaka alimweleza Waziri huyo wa Uwekezaji kuwa Uongozi wa kiwanda hicho uliamua kuongeza jumla ya vibarua 200 kutokea Burundi ili kukidhi mahitaji ya ujenzi kumalizika kwa wakati Kutokana na Wanyausi kushindwa kufanya kazi inavyohitajika.
Mtaka alieleza kuwa ufanyaji kazi wa vibarua wengi Wazawa umekuwa wa kusua sua kwani wanapofanya kazi kwa wiki moja hupenda kupumzika kwa wiki nyingi mfululizo kutokana na kuridhika na kipato hicho kidogo jambo linaloonekana kukwamisha ujenzi wa kiwanda hicho.
"Dodoma ni makao makuu,kuna fursa
nyingi,sisi kama Serikali tunaumia kuona Vijana wetu wanakosa fursa halafu
wageni wanapewa eti kwa sababu ya uvivu,naahidi mimi na kamati yangu tutakaa na vijana wetu tuwaelekeze cha kufanya,nadhani
hii itasaidia kuondokana na vibaka ,"anasisitiza Mkuu huyo wa mkoa a Dodoma.
@
Social Plugin