WATU 5000 KUPATIWA MATIBABU BURE


Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Kigoma wakihojiwa na kufanyiwa vipimo vya awali kabla kupelekwa kwa madaktari ili kuendelea na taratibu za matibabu. (Picha na Fadhili Abdallah)
Wananchi wa wilaya ya Kigoma waliojitokeza kwenye mpango wa matibabu bure yanayotolewa na Taasisi ya Al Ataar Charitable foundation kwa ufadhili wa Qatar Foundation, matibabu hayo yanfanyika hospitali ya mkoa Kigoma Maweni kwa siku tatu.
***

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

ZAIDI ya watu 5000 wanatarajia kufikiwa katika huduma za matibabu bila malipo yanayotolewa na taasisi ya Al Ataa Charitable Foundation kwa ufadhili wa Qatar Charity.


Mkurugenzi Mtendaji wa Al Ata’a Charitable Foundation, Shekhe Ahmed El Hamrany alisema hayo katika kambi ya matibabu bila malipo inayoendeshwa na taasisi hiyo kwenye hospitali ya mkoa Kigoma Maweni kwa muda wa siku tatu mfululizo.


Shekhe Hamrany alisema kuwa kwa mwaka huu katika mipango yao watakuwa na jumla ya kambi 11 kwa ajili ya kusaidia huduma za matibabu bila malipo katika maeneo mbalimbali nchini na kwamba lengo ni kusaidia jamii yenye kipato duni kupata huduma za matibabu.


Alisema kuwa miongoni mwa magonjwa yanayoshughulikiwa kwenye mipango hiyo ni pamoja na upimaji wa magonjwa ya moyo, magonjwa ya mfumo wa upumuaji, macho, kisukari na magonjwa mengine ambayo yatajitokeza.


Katika hilo alisema kuwa pamoja na kufanya uchunguzi na upimaji wa magonjwa lakini pia wanatoa dawa, operesheni kwa magonjwa yanayoweza kufanyiwa operesheni kwenye hospitali za mikoa na wanaohitaji operesheni kubwa wanapewa rufaa kwenye hospitali ambazo zinatoa operesheni za magonjwa hayo.


Baadhi ya wananchi waliohudhuria kwenye mpango huo wa matibabu bila malipo walisema kuwa wanajitokeza kwa wingi wanaposikia matangazo kuhusu kuwepo kwa kambi hizo za matibabu kutokana na uwezo mdogo walionao hivyo uwepo wa kambi hizo unawasaidia kupata upimaji na matibabu.


Salewa Hamisi Mkazi wa kijiji cha Mahembe Kigoma Vijijini alisema kuwa watu wengi vijijini hawana uwezo wa gharama za kumudu vipimo lakini pia kumudu dawa na upasuaji wa magonjwa makubwa ambayo yanatesa watu wengi vijijini ambako hakuna kabisa huduma hizo.


Naye Rashidi Kilaule mkazi wa Gungu Manispaa ya Kigoma Ujiji alisema kuwa watu wengi ni wagonjwa na wanahitaji upimaji na matibabu lakini wengi hawawezi kumudu gharama hivyo kunatokea vifo vingi vijijini kwa watu wengi kushindwa kumudu gharama za kusafiri lakini pia kugharamia huduma hizo za matibabu.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post