AJALI YA TRENI YA ABIRIA YAUA NA KUJERUHI 205 TABORA


Mabehewa sita ya Treni ya abiria Treni ya Abiria namba Y14 yenye Injini namba 9019 iliyokuwa ikisafiri kutoka Kigoma kuelekea Tabora Mpaka Dar es salaam yameanguka leo Jumatano Juni 22, 2022 katika eneo la Kata ya Malolo iliyopo katika manispaa ya Tabora na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa.

Inaelezwa kuwa Treni hiyo iliondoka stesheni ya Kigoma saa mbili usiku Jumanne Juni 21, 2022 kuelekea Dar es Salaam ikiwa na behewa nane zilizobeba abiria 930 na ilipofika eneo la malolo kilomita 10 kutoka stesheni ya Tabora, behewa tano za abiria daraja la tatu, behewa moja la vifurushi, behewa moja la huduma ya chakula na vinywaji na behewa la breki yalianguka na kusababisha ajali.

Wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) likisema watu wanne wamefariki na wengine 132 kujeruhiwa katika ajali ya treni iliyotokea leo eneo la Malolo mkoani Tabora, mkuu wa Mkoa wa Tabora amesema waliofariki ni watatu na majeruhi ni 205.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na TRC kupitia mkuu wa kitengo cha habari na uhusiano TRC, Jamila Mbarouk, inaeleza kuwa watu wanne wamefariki na majeruhi 132 walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa ya Kitete- Tabora kwa ajili ya matibabu.

“Kati ya waliofariki wapo watoto wawili, mmoja wa kike ana umri wa miaka mitano na wa kiume ana miezi minne na watu wazima wawili, mwanaume na mwanamke,” imeeleza taarifa hiyo.

Muda mchache baadaye mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Batilda Burian amesema waliofariki ni watatu na 205 wakijeruhiwa katika ajali hiyo.

Mkurugenzi wa TRC, Masanja Kadogosa amesema chanzo cha ajali ni hujuma iliyofanywa katika miundombinu ya reli ambapo kuna kipande cha reli kiliondolewa katika eneo hilo na kisha kurudishwa kwa kuegeshwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post