TUNDU LISSU : SERIKALI IMENILIPA MADENI YANGU..'KIINUA MGONGO...NI JAMBO JEMA KWA KWELI

 


Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu amesema Serikali imemlipa kiunua mgongo chake aliochukuwa akikidai baada ya kutumikia nafasi ya ubunge kwa zaidi ya miaka mitatu.

Wakati Lissu akisema amelipwa madeni hayo,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Emmanuel Tutuba amesema ni utendaji wa kawaida serikalini kulipa madeni ya wafanyakazi na viongozi hata mafao ya wastaafu.

Lissu aliyekuwa mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alivuliwa ubunge Juni 28 mwaka 2019 kwa madai mbalimbali yakiwemo ya kutojaza taarifa za mali na madeni na sababu ya pili kutokutoa taarifa kwa Spika mahali alipo.

Wakati huo, Lissu alikuwa Ubelgiji akiendelea na matibabu baada ya kupigwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma. Licha ya kufanya juhudi mbalimbali za kufuatilia kiunua mgongo chake Lissu hakufanikiwa.

Lakini Februari mwaka huu, alipokutana na Rais Samia Suluhu Hassan Ubelgiji Lissu alifikisha kilio hicho kwa mkuu huyo wa nchi, ambaye alimuahidi kumsadia kulitatua. Pia Lissu alimuomba Rais Samia kumsaidia kupata hati ya kusafiria, jambo lilitekelezwa ndani ya muda mfupi na Serikali.

Akizungumza na mmoja wa mtandao  Jumatano Juni Mosi 2022, Lissu amesema kuwa miezi miwili iliyopita alipigiwa simu na mtu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango akamueleza kuwa madeni aliyokuwa akidai yameshalipwa.

“Nilikuwa na madeni ambayo nilikopa katika benki mbili na nilishtakiwa na mojawapo ya benki kwa kushindwa kulipa mkopo uliokuwa unalipwa kupitia mshahara wa ubunge. Nilipelekwa mahakamani na benki hiyo.

“Alivyonipigia simu akaniambia nimelipiwa madeni yangu yote kutokana na kiinua mgongo. Naweza nikasema hadharani kwamba limefanyiwa kazi ni jambo jema kwa kweli. Sina madeni ya benki na usumbufu niliokuwa nikiupata,” alisema Lissu.

Alipoulizwa kwa njia ya simu simu kuhusu Lissu kulipwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Emmanuel Tutuba amesema “Tunapolipa huwa tunapeleka kwa ofisa masuuli wa taasisi husika. Kwa mbunge, kuna mfuko wa Bunge. Pesa zinapelekwa huko.

“Hata hizo za matibabu zinaingizwa huko pia. Ukiwasiliana na Bunge watakuwa na taarifa zaidi kwa sababu wao ndio wanaowajua wanaostahili,” amesema Tutuba.

Kwa mujibu wa Lissu, maombi mbalimbali aliyoyafikisha kwa Rais Samia yamefanyiwa kazi, kwa kiasi kikubwa ikiwemo kuachiliwa huru kwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na wafungwa wa kisiasa waliokuwa katika magereza mbalimbali.

Lissu alisema watu wengi wameachiwa na kesi nyingi zilizokuwa mahakamani zimefutwa, ingawa bado zipo kesi za makada wa Chadema zipo mikoa ya Njombe na Songwe, hata hivyo zinashughulikiwa na zitaisha.

Hata hivyo, ambaye ni mbunge wa zamani wa Singida Mashariki haki za matibabu na usalama wake pindi atakaporejea Tanzania ni miongoni mwa mambo bado hayajafanyiwa kazi. Ingawa alisema kuhusu matibabu alitakiwa kuandika barua.

“Nililetewa ujumbe niandike barua kuomba nilipe stahiki zangu za matibabu na nimeshaiandaa kukamilika kwa kiasi kikubwa ingawa bado natafuta nyaraka kwa sababu nimetibiwa Kenya na Ubelgiji.

“Kwa sasa nakusanya nyaraka zote hili nizipeleke pamoja na barua, kwa sababu Rais Samia aliniahidi kulishughulikia. Suala la usalama wangu nilimuomba Rais Samia atoe tamko la kusema Lissu na wenzake waliokimbia nchi wakirudi Tanzania kwamba mkuu huyo nchi ndio msalaba wao kwa lolote litakalotokea,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post