TCB YAONYA MATUMIZI YA HIRIZI UNUNUZI WA PAMBA

 

Na Daniel Limbe, Chato

SERIKALI kupitia Bodi ya pamba nchini (TCB) imewaonya viongozi wa Amcos zinazonunua pamba nchini, kuacha kutumia hirizi kwenye mizani ya kupimia pamba kwa lengo la kuwaibia wakulima.


Mbali na hilo, njia zingine ni pamoja na kutumia boriti za baiskeli, kukata siri za mzani, pamoja na kurudisha nyuma mishale ya kuhesabia uzito ndani ya mizani inayotumika kununulia pamba mbegu kutoka kwa wananchi.


Mkaguzi wa Bodi ya wa pamba(TCB) wilaya ya Chato na Biharamulo mkoani Kagera, Samweli Mdidi, ametumia fursa hiyo kuwaonya viongozi wa Amcos 53 zinazounda ushirika wa Chama kikuu cha CCU kutorudia kufanya makosa ya makusudi kama waliyofanya katika msimu wa ununuzi wa pamba wa 2021/22.


"Mwaka jana kuna amcos zilifanya mambo yasiyoruhusiwa katika ununuzi wa zao la pamba, ambapo kuna kituo kimoja cha ununuzi wa Pamba(jina tunalihifadhi) tulibaini mzani waliokuwa wanatunia walikuwa wameufungia hirizi" amesema Mdidi.


Kutokana na hali hiyo,amesema kwa msimu huu wa 2022/23 serikali kupitia Bodi ya pamba itawachukulia hatua wote watakao kiuka masharti ya ununuzi wa pamba ikiwa ni pamoja na kutozwa faini zilizoainishwa kwa mujibu wa sheria za bodi hiyo.


Ofisa kutoka wakala wa vipimo (WMA)mkoa wa Geita, Lusako Mwaipaja, amesema kitendo cha kuchezea vipimo (Mizani) kukata siri, kukata gia, kutumia vipimo ambavyo havijathibitishwa na mamlaka hiyo pamoja na kumzuia mkaguzi kufanya kazi yake ni kosa kisheria.


Aidha amesema iwapo mtu atathibitika kufanya moja ya makosa hayo adhabu kali za mamlaka hiyo huchukuliwa ikiwa ni pamoja na kutozwa faini ya kuanzia shilingi milioni 1 hadi sh. 20 milioni.


Na kwamba iwapo mtuhumiwa atafikishwa mahakamani na kuthibitika kutenda kosa hutozwa faini isiyopungua shilingi laki 1 na isiyozidi 40 milioni.


Kwa upande wake Meneja wa Chama kikuu cha ushirika CCU,Berino Msigwa, amewataka viongozi wa Amcos hizo kubadilika ki fikra ili kujenga uaminifu kwa wakulima, kwa madai iwapo wataendelea kuwahujumu wakulima kwa kuwapunja mazao yao huenda wakapoteza ajira hiyo kama ilivyojitokeza kwa baadhi ya mikoa hapa nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post