Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

FAMILIA YAGOMA KUONDOA KABURI KATIKATI YA BARABARA BARIADI..MKUU WA MKOA DAVID KAFULILA AINGILIA KATI




Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila (aliyeshika kiuno) akimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange (mwenye kofia) akimwelezea namna changamoto ya kaburi kuwa katikati ya barabara kijiji cha Nkindwabiye.

Na Constantine Mathias, Bariadi.

Familia ya Saguda Madako katika kijiji cha Nkindwabiye Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, imegoma kuhamisha kaburi linalodaiwa kuzikwa mama yao mzazi ambalo lipo katikati ya Barabara katika kijiji hicho kwa madai hadi walipwe kiasi cha Shilingi Milioni 30 na serikali.


Kaburi hilo limejengwa katikati ya Barabara kuu ya Nkololo-Byuna- Nkindwabiye–Halawa, ambapo familia hiyo imedai mama yao mzazi alizikwa eneo hilo tangu mwaka 1974, na kujengelewa mwaka 2006.


Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa huo David Kafulila wakati akikagua ujenzi wa Barabara hiyo, Meneja Tarura Wilaya, Mhandisi Mathias Mgolozi amemweleza Mkuu huyo wa Mkoa kuwa licha ya kukaa na familia hiyo mara kwa mara kwa ajili ya kuhamisha kaburi hilo lakini imeshindikana.


Mgolozi amesema mara ya kwanza familia hiyo ilitaka Milioni 30 ili kaburi hilo lihamishe, baadaye wakataka Milioni 20, na mara ya mwisho walipunguza na sasa wanahitaji Milioni 1.5.


“Baada ya madai hayo, tulimweleza kwa mujibu wa sheria kuhamisha kaburi familia inapewa kiasi cha Sh. 500,000 na serikali itasaidia kuhamisha kaburi hilo, lakini mpaka sasa familia imegoma,” amesema Mhandisi Mgolozi.


Baada ya hali hiyo Mkuu wa Mkoa, aliagiza kuhamishwa kwa kaburi hilo bila ya kusikiliza uamuzi wa familia kama inataka au hapana na familia ipewe kiasi hicho cha pesa kama sheria inavyotaka.


“Kama sheria inasema hivyo basi naagiza kaburi hili liondolewa mara moja, endapo ujenzi wa Barabara hii utaaanza kaburi liondolewa familia ikubali isikubali kaburi liondolewe na ujenzi wa barabara ufanyike,” amesema Kafulila.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com