Kamanda wa polisi mkoa Kigoma James Manyama (wa pili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kigoma.
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Jeshi la polisi mkoa Kigoma limebaini viungo vya binadamu vilivyokamatwa Mkoani humo Juni 3,2022 ni viungo vya Bilihanyuma Suminda, mzee mwenye miaka 90 ambaye alizikwa mwezi Januari mwaka huu.
akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma
Akitoa muendelezo wa taarifa ya watu waliokamatwa na viungo vya binadamu Juni 3 mwaka huu Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, James Manyama amesema kuwa polisi wamefukua kaburi la mtu ambaye viungo hivyo vilifukuliwa na kuthibitisha kuwa vilikuwa ni viungo vya Bilihanyuma Suminda, mzee mwenye miaka 90 ambaye alizikwa mwezi Januari mwaka huu.
Kamanda huyo wa polisi amewataja watuhumiwa hao akiwemo Bankana Zakayo (41) aliyekuwa Sengerema mkoa Mwanza ambaye alikuwa akipelekewa viungo hivyo na Miraji Nyambi (45) aliyekuwa dereva wa gari lililokamatwa na viungo hivyo ambao wote ni walimu wa shule ya sekondari Mwandiga wilaya ya Kigoma.
Sambamba na hao amewataja pia Mathayo Ndayishimiye (40) Mganga wa kienyeji kutoka nchini Burundi, Ramadhani Abrahaman (52) Mganga wa kienyeji, Adizino John (62), Nguno Manyanza (49), James Kibeba (68), Kelvin Fedha na Thobias Fundo (33).