Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KILI CHALLENGE 2022 KUANZA KUTIMUA VUMBI JULAI 15


Baadhi ya waendesha baiskeli watakaoshiriki kampeni ya GGML Kili Challenge kwa kupanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kukusanya fedha za kutunisha mfuko wa kutokomeza maambukizi ya VVU na Ukimwi.
***

Mashindano ya Kill Challenge 2022 yanayoratibiwa na Kampuni ya Geita Gold Mine Limited (GGML) yanatarajia kuanza kutimua vumbi Julai 15 mwaka huu yakianzia geti la Machame na kuhitimishwa katika geti la Mweka tarehe 21 Julai 2022.


Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Meneja wa Kilimanjaro Challenge Against HIV and AIDS Trust, Manace Ndoroma, alisema mashindano hayo yamepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 hadi kuwa mashindano ya kimataifa, yenye kushirikisha zaidi ya wapanda mlima 500 kutoka mabara 6 na zaidi ya nchi 20 na kukusanya zaidi ya dola milioni 2 hadi sasa.


"Wewe pia unaweza kujiunga na timu yetu ya wapanda farasi na wapanda baiskeli kwa mwaka huu 2022 ili kutusaidia kuchangisha pesa. Unawez kuona namna ambavyo kiasi kidogo utakachochangia kinavyoweza kubadilisha maisha ya mtu mwingine.


Aliongeza, “athari za VVU/UKIMWI kwa Watanzania bado ni mbaya kwani wazee wengi masikini wanalazimika kuwalea watoto wadogo baada ya kufiwa na wazazi wao kutokana na ugonjwa huu. Familia hizi nyingi hazina uwezo wa kifedha wa kuwategemeza watoto hawa, na nyingi zimeachwa bila chakula, maji au matibabu.”


Ndoroma alisema tangu kuanza kwa msafara wao wa kwanza wa mashindano hayo mwaka 2002, idadi ya maambukizi mapya nchini Tanzania yamepungua zaidi ya nusu.


“Mgawanyo wa fedha kwa walengwa mbalimbali umekuwa muhimu katika dhamira yetu ya kufikia “sifuri tatu” kwa kuboresha miundombinu kupitia ujenzi wa vituo vya kulelea watoto yatima, shule, zahanati na vituo vya ushauri nasaha, pamoja na ukarabati wa vituo vya matibabu vya ndani na mikoa,” alisema.


Aliongeza kuwa fedha hizo zilisaidia kuongeza ufikiaji wa huduma za kupima, kutibu, na ushauri kwa watu walioambukizwa na jamii zao.


Mwaka 2002, AngloGold Ashanti – Geita Gold Mine ilizindua mashindano hayo kwa ushirikiano na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).


Mashindano ya Kili Challenge hufanyika kila mwaka kuchangisha fedha ambayo inasaidia mpango wa serikali ya Tanzania nchi nzima wa kutokomeza maambukizi mapya ya VVU, unyanyapaa na ubaguzi na vifo vinavyohusiana na UKIMWI.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com