Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akifungua mafunzo ya namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama kwa Mahakimu 43 kutoka Mikoa Mbalimbali ya Tanzania yanayofanyika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akifungua mafunzo ya namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama kwa Mahakimu 43 kutoka Mikoa Mbalimbali ya Tanzania yanayofanyika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Washiriki wa Mafunzo ya namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama wakiendelea na mijadala mbalimbali katika mafunzo hayo.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Richard Kabate akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo katika picha ya pamoja na Mhe. Wilbert Chuma, (Mgeni Rasmi) wakiwa ameketi na Hakimu Mfawidhi wa Wilaya Lushoto, Mhe. Rose Ngoka na Kaimu Mkuu wa Chuo Bw. Goodluck Chuwa (upande wake wa kulia) na Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha Na Utawala, Prof. Fatihiya Massawe na Naibu Mkurugenzi wa Utawala, Mahakama ya Tanzania na Mratibu wa Mradi wa BSAAT nchini Bwn. Stephen Magoha (Upande wa Kushoto)
Na Ibrahim Mdachi – IJA Lushoto
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania chini ya ufadhili wa Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Tanzania zinazohusika na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (BSAAT) kimeendesha mafunzo ya siku tatu kwa Mahakimu 43 kuhusu namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri za Mahakama. Mafunzo hayo yalianza tarehe 13 Juni, na kuhitimishwa tarehe 15 Juni, 2022 Chuoni hapo.
Akifungua mafunzo hayo rasmi, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma aliwataka Mahakimu kuzingatia mwongozo wa adhabu na kujiepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kujenga jamii inayojali haki kwa kila mmoja na kuwafanya wananchi waendelee kuwa na imani na Mahakama.
Alitanabaisha pia kuwa kimsingi mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo na uelewa wa mwongozo wa utoaji adhabu ambao ni miongoni mwa nyenzo za maafisa wa Mahakama katika mchakato wa utoaji wa adhabu kuwa halali na usiotiliwa shaka na wadaawa wanaohusika katika mashauri mahakamani wakiwemo washtakiwa, waathiriwa, wapelelezi, mawakili wa utetezi, waendesha mashtaka na umma kwa ujumla.
Mhe. Chuma alisema kuwa ni matarajio ya Mahakama ya Tanzania kupitia mafunzo hayo washiriki watapata uelewa wa mwongozo wa utoaji adhabu, hivyo kutumika ipasavyo katika mashauri hasa ya rushwa, uzoefu utakaopatikana utafikishwa kwa maafisa wengine wa Mahakama ambao hawakufanikiwa kupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Mratibu wa Programu ya BSAAT ya Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha akitoa maelezo mafupi kuhusu mradi huo alisema kuwa, program hiyo inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kwa kushirikana na Umoja Ulaya (EU) na kuratibiwa na Ofisi ya Rais, Ikulu ilianza kutekelezwa mwaka 2018/2019 ikijumuisha taasisi tisa nufaika ambazo ni wadau katika mnyororo wa haki jinai ikiwemo Mahakama kama mdau muhimu katika utiaji wa haki.
Bw. Magoha aliongeza kuwa program hiyo imelenga kupunguza vitendo vya rushwa kama kikwazo cha kupunguza kiwango cha umasikini kwa Watanzania, kuboresha uadilifu, kuboresha uwezo na uratibu wa mfumo wa haki jinai katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa na kuongeza imani kwa umma juu ya utendaji kazi wa Mahakama.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo Bw. Goodluck Chuwa alisema kuwa, ni takribana miaka mitano tangu chuo kimeamua kujikita katika kutimiza malengo yake ya msingi ya kuundwa kwake kitahakikisha kuwa kinaendelea kuyaratibu mafunzo mbalimbali kwa weledi mkubwa kwa lengo la kuleta tija kwa Mahakama na wadau wengine wa sheria nchini.
Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021-2025, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja na Mpango Mkakati wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto wa miaka mitano wa mwaka 2018-2023.
Social Plugin