Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongella ametuma salamu kwa aliyehusika katika mauaji ya askari wilayani Ngorongoro, katika zoezi la uwekaji mipaka katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo.
Mongella amesema aliyefanya tukio hilo ajisalimishe kituo cha Polisi vinginevyo ajue hayuko salama, atakamatwa tu.
Amesema hayo leo June 12 2022 wakati wa kuaga mwili wa marehemu Garlius Mwita eneo la Loliondo wilaya ya Ngorongoro ambapo mwili umeagwa kuelekea nyumbani kwao Musoma Mkoa wa Mara.
Jana Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela alithibitisha kuuawa kwa askari wa Jeshi la Polisi baada ya kupigwa mshale katika eneo la Loliondo wakati akiendelea kutekeleza majukumu yake ya ulinzi na usalama.
Aidha John Mongela alithibitisha kuwepo kwa amani ya kutosha na kuwataka wanaosambaza taarifa za uongo mitandaoni waaache mara moja.
RC Mongela alisema kumekuwa na upotoshwaji wa makusudi wa kutumia baadhi ya picha ambazo nyingi ni za miaka mitatu au minne iliyopita.
Wakati huohuo RC Mongela alibainisha kuwa mbali na kifo hico hakuna majeruhi mwingine yeyote yule kwenye hospitali zote za Mkoa wa Arusha anayehusika na tukio la Loliondo.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa rai kama kuna mwananchi yeyote aliyejeruhiwa na vyombo vya ulinzi na usalama basi ajitokeze apewe huduma kwani Serikali ya awamu ya 6 ni Serikali sikivu na inaendeshwa kwa utawala wa sheria na demokrasia.
Social Plugin