Leo Juni 22, 2022 Mahakama Kuu imetupilia mbali kesi ya msingi iliyofunguliwa na wabunge 19 wa viti maalum CHADEMA waliovuliwa uanachama na chama chao la kupinga kuvuliwa uanachama na Baraza Kuu la CHADEMA.
Chadema iliwafukuza rasmi wabunge hao Mei 12, 2022, kwenye mkutano wao mkuu uliofanyika Mlimani City ambapo baada ya hapo walifungua kesi ya pingamizi katika mahakama kuu ambayo ndiyo imetolewa maamuzi leo.
Wabunge hao 19 wa Chadema waliingia bungeni baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ambapo Chadema ilijitokeza hadharani mara kadhaa kukanusha kuwa sio wabunge wao na kwamba hawakuwasilisha majina ya wabunge wao wa viti maalum.
Akizungumza na vyombo vya habari mbele ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakili wa CHADEMA Peter Kibatala, amefafanua kuwa Mahakama pia imetupilia mbali maombi ya msingi ya kutaka kupewa kibali cha kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama.
Aidha Kibatala ameeleza kuwa miongoni mwa sababu ya kutupiliwa mbali kwa maombi hayo ni kukosewa kwa jina la mjibu maombi namba moja ambaye ni Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA iliyosajiliwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, ameomba sasa sheria kufuata mkondo wake, akibainisha kwa sasa hawaoni sababu ya wabunge hao kuendelea kusalia bungeni.
Social Plugin